Sambaza....

MIAKA miwili iliyopita timu ya Taifa ya Visiwa vya Cape Verde ilikuwa miongoni mwa Mataifa matatu bora katika viwango vya soka barani Afrika, na Ijumaa hii timu ya Taifa ya Tanzania ´Taifa Stars´ itaikabili nchi hiyo ndogo ya Magharibi mwa Afrika katika mchezo wa kundi la saba kuwania tiketi ya kufuzu CAN2019-Cameroon.

Stars ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi-alama mbili tofauti dhidi ya vinara Uganda. Baada ya sare ya kufungana 1-1 na Lesotho katika mchezo wa kwanza jijini, Dar es Salaam, Stars ilisafiri hadi Uganda na kulazimisha suluhu-tasa na sasa ndani ya siku nne kuanzia Ijumaa hii kila kitu kinaweza kuwa wazi-kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 38, ama kuendelea kusubiri.

MBWANA SAMATTA.

Ndiye kinara wa ufungaji magoli katika ligi kuu Ubelgiji msimu huu. Jumapili iliyopita alifunga goli lake la saba katika ligi wakati KRC Genk iliposhinda 5-1 ugenini dhidi ya KAA Gent. Kiujumla, Samatta anakwenda kuwabili Cape Verde Ijumaa hii akiwa amefunga magoli 14 klabuni Genk.

Magoli saba katika Europa League (sita akifunga katika hatua ya mtoano- ikiwemo Hat Trick yake ya kwanza katika michuano ya ulaya dhidi ya Brondby ya Denmark) na moja katika hatua ya makundi walipoichapa Malmo FF ya Sweden mwezi uliopita. Anaenda kuongoza mashambulizi ya Stars akitoka kufunga Hat trick mbili- ikiwemo dhidi ya Zulte Wargen siku 13 zilizopita.

Takwimu zake klabuni msimu huu ni bora kuliko kipindi chochote cha uchezaji wake na pengine kinawakumbusha baadhi ya watu ubora wake wakati angali kinda U18 mwaka 2009 alipofunga jumla ya magoli 15 katika michezo 16 ya ligi daraja la kwanza Tanzania bara na kuisaidia Mbagala Market ( sasa African Lyon) kupanda ligi kuu kwa mara ya kwanza.

Akiwa tayari amefunga goli moja katika kampeni ya kufuzu CAN ijayo, Samatta anapaswa sasa kuibeba zaidi Stars katika mabega yake hata kama ni kweli hapati huduma nzuri kiuchezaji. Ndivyo wafanyavyo Leo Messi na Cristiano Ronaldo katika nchi zao za Argentina na Ureno.

Ni ukweli ulio wazi kwamba huduma wanazopata Messi na Cristiano kiuchezaji katika timu zao za Taifa hazifanani na zile wazipatazo klabuni lakini tazama, Messi aliibeba Argentina na kuifikisha fainali tatu mfululizo kubwa-kombe la dunia 2014, Copa America 2015 na 2016, wakati Cristiano alisaidia ubingwa wa Uefa Euro 2016 kwa Ureno.

Kuna baadhi ya wadau wamekuwa wakimkosoa Samatta na kusema HAJITOLEI ipasavyo katika timu ya Taifa- labda ni kweli kwasababu takwimu zake kiufungaji akiwa Stars ipo chini. Kwa misimu mitano aliyochezea TP Mazembe ya DR Congo alifunga magoli yasiyopungua 80 na maendeleo yake Genk tangu Januari 2016 yamefanya wengi kuhoji mchango wake akiwa Stars.

Si kwamba hafungi akiichezea Stars lakini watu wanataka kumuona akifanya hivyo mara kwa mara hasa katika mipambano muhimu kama hii miwili ijayo vs Cape Verde Islands, na si kusubiri goli moja ama mawili kwa mwaka.

Samatta alipoteza nafasi ya kufunga dhidi ya Uganda mwezi uliopita wakati kipa wa Cranes , Denis Onyango alipotokea na kuliacha mbali lango lake. Nafasi zile Samatta huzigeuza magoli akiwa TP na huko Genk, ndiyo maana husemwa HAJITOLEI akiwa Stars.

Sambaza....