Baada ya Ligi Kuu nchini Uingereza kusimama kwa muda mrefu kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa corona sasa Ligi hiyo pendwa duniani inarudi kukipiga kama kawaida.
Epl inarejea leo baada kupita ya siku kadhaa bila kuchezwa, ambapo leo itapigwa michezo miwili ya ufunguzi baada ya urejeo wake. huku chama la nahodha Mbwana Samatta wa timu ya Taifa ya Tanzania likipambana kutokushuka daraja.
Aston Villa watafungua dimba kwa kuikaribisha Sheffield United katika uwanja wake wa Villa Park. Mpaka sasa Aston Villa inashika nafasi ya 19 kwenye msimamo ikiwa na alama 25 katika michezo 28 iliyoshuka dimbani, Sheffield Utd wao wapo katika harakati za kutafuta nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya wakiwa nafasi ya 7 na alama zao 43.
Mchezo wa pili ama mchezo wa siku ni kati ya Arsenal dhidi ya Manchester City ambapo Mikel Arteta atakutana na bosi wake wa zamani Pep Guardiola. City imeshakata tamaa ya ubingwa na kukubali yaishe mbele ya Liverpool. Man City sasa wanatafuta heshima na kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Liverpool wakati Arsenal bado wana matumaini ya kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kumaliza ndani ya nne bora.