Sambaza....

Mwishoni mwa juma hili kutakuwepo na derby ya kirafiki, derby ambayo mashabiki wa timu zote mbili hukaa pamoja na kushangilia pamoja bila vurugu yoyote.

Hakuna uhasama kwenye Merseyside derby, derby ambayo mfalme wake ni Ian Rush, magoli 25 aliyoyafunga kwenye derby hii yanamfanya kuwa mchezaji aliyefunga magoli mengi kwenye mechi ya Liverpool na Everton.

Uimara wa miguu yake ulifanikisha kuweka rekodi hii, rekodi ambayo hakutosheka nayo katika maisha yake ya mpira, akaamua kuwekeza juhudi za ufungaji mpaka akaifungia Liverpool magoli 346 magoli ambayo yalimfanya kuwa mfungaji bora wa wakati wote wa Liverpool mbele ya Roger Hunt.

Uhai wa soka wa Roger Hunt ushafikia kikomo, hawezi tena kuifikia au kuivunja rekodi ya Ian Rush, kinachobaki ni pengo kubwa la magoli 60, magoli ambayo hatoweza kuyafikia tena kwa sababu kwa sasa viatu vyake vimezeeka.

Viatu vipya ndivyo vinavyofikiriwa kufikia rekodi ya Ian Rush, tulitamani kumuona Michel Owen akifika lakini pesa za Real Madrid zilituharibia matamanio yetu.

Siku zilipozidi kukimbia zilifanikiwa kumfikia Fernando Torres ambaye tulimuona anaweza akafikia rekodi ya kina Ian Rush na Roger Hunt, lakini kama ilivyokuwa kwa Michel Owen, pesa tamu za Chelsea zikaharibu kila kitu tulichokuwa tunakifikiria.

Tulifikiria Liverpool itakuwa timu ya kupigania makombe makubwa tena, irudi kwenye zama zake ili wachezaji nyota waweze kubaki ndani ya timu na kuvunja rekodi za watu wengi, lakini ilikuwa tofauti utajiri wa makombe ya Barcelona ulimshawishi Luiz Suarez kuondoka Anfield.

Anfield ƙlikawa daraja la wachezaji nyota kupita na siyo kukaa tena. Pesa na Makombe yakawa yanafupisha safari ya wachezaji nyota waliokuwa wanaibuka Liverpool.

Maumivu yakawa ndani ya mashabiki wa Liverpool, hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na hali. Mwenendo wa timu yao ulikuwa mbovu.

Hata alipoondoka Philipe Countinho watu walisonya sana, wakatukana sana , wakachoma jezi yake lakini vyote hivo havikutosha kufuta ukweli kuwa Philipe Countinho alikuwa ameshahama Liverpool na kuipenda jezi ya Barcelona.

Inawezekana Mohamed Salah alitumika kama mtu wa kuwasahaulisha maumivu ya kuondokewa na Philipe Countinho.

Magoli yake yalikuwa leso ya kufuta machozi ya mashabiki wa Liverpool, usoni mwao wakawa na tabasamu pana lakini tabasamu hili ni la mashaka kwa sababu hawajui kama Mohamed Salah atatumia Anfield kama daraja au kama makazi ya muda mrefu.

Makazi ambayo yatamfanya awe mfalme mpya pale kwa sababu ana viatu vipya vinavyoweza kufikia rekodi za kina Ian Rush na Roger Hunt.

Watu watakukumbuka kwa alama ambazo umeacha sehemu fulani, Ian Rush na Roger Hunt waliwahi kuacha alama za kufunga magoli 40 ndani ya msimu mmoja, alama ambayo Mohamed Salah anaelekea kuifikia.

Magoli 37 mpaka sasa tena katika msimu wake wa kwanza na Liverpool, hii ni dalili tosha anaweza kufikia alama nyingi zilizowahi kuwekwa na Ian Rush pamoja na Roger Hunt.

Kinachotia kigugumizi ni hii hali iliyopo Liverpool, wachezaji nyota wengi huitumia Liverpool kama sehemu ya kupitia na siyo sehemu ya kukaa.

Mohamed Salah ataweza kukaa Liverpool muda mrefu na kujiwekea ufalme wake wa kudumu? Ana ubavu wa kuikataa Ofa za Barcelona na Real Madrid zitakapokuja mezani kwake? Timu ambazo zinaweza kumpa uhakika wa kushinda klabu bingwa ulaya? Timu ambazo zinaweza kusukuma mafanikio yake binafsi kwenye tunzo mbalimbali?

Haya ni maswali magumu na mazito, maswali ambayo yanazika matamanio yangu ya kumuona Mohamed Salah alipowahi kufikia Ian Rush na Roger Hunt

Natamani sana Mohamed Salah aamini ninavyoamini mimi kuwa popote unaweza ukapafanya pawe nyumbani kwako penye furaha.

Uwezo wake uliopo ndani ya miguu yake ni silaha tosha ya kuweka furaha moyoni mwake, kitu kizuri yuko chini ya kocha mshindi Jurgen Klopp, ni rahisi kwake kupafanya Liverpool kuwa sehemu yenye furaha na kufikia walipowahi kufika kina Roger Hunt na Ian Rush

Sambaza....