Usajili ni kamari, ni kama mchezo wa kubahatisha hivi kwani baadhi ya wachezaji husajiliwa wakiwa na viwango na ufanisi mkubwa lakini wakienda katika timu au ligi nyingine hushindwa kufanya vizuri na wengine hufanya vizuri zaidi.
Kufeli kwa baadhi ya sajili katika ligi yetu sio la Tanzania pekee kwani wapo baadhi ya wachezaji wakubwa husajiliwa na kushindwa kufanya vizuri na kuonyesha makeke katika timu zao mpya walizosajiliwa.
Mfano pale barani Ulaya ambapo soka linapigika kwelikweli, wapo baadhi ya wachezaji wameshindwa kufanya vizuri baada ya kuhama timu zao na kusajiliwa katika timu mpya, mfano Eden Hazard alisajiliwa na Reel Madrid mwaka 2019 akitokea Chelsea akiwa wamoto kwelikweli lakini alipohamia Real Madrid alishindwa kufanya vizuri kwani ndani ya miaka minne aliyokaa pale Los Blancos alifanikiwa kufunga magoli manne pekee.
Kama inavyofahamika kwamba usajili ni kamari ngumu lakini wataalamu wa usajili(scouts) hutizama usajili kama kamari ya ushindi, wanaamini usajili ni kete ya ushindi wakiamini kuwa bila kufanya usajili basi ni vigumu kushindana na timu kubwa katika mashindano makubwa. Hivyo vilabu hulazimika kuingia sokoni kutafuta wachezaji.
Katika ligi ya Tanzania zipo sajili kadhaa kubwa zilishindwa kulipa matunda na matokeo chanya kama ilivyokusudiwa na kufeli kwa sajili hizo kukisabishwa na baadhi ya mambo kama vile umasikini wa vilabu vyetu hivyo huwalazimu kununua wachezaji wa bei ndogo na wenye viwango vidogo, kutokuwepo kwa vitengo vya usajili(scout) n.k.
Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ambayo yatazisaidia timu zetu za Tanzania ili kupata manufaa makubwa ya usajili.
Uundaji vitengo maalumu vya usajili (scouts). Hivi karibuni klabu ya Simba ilitangaza kuanzisha kitengo cha “scout” ambacho kinafanya kazi sambamba na benchi la ufundi, na hii inasaidia kurahisisha upatikanaji wa wachezaji wa sifa wanazotaka benchi la ufundi.
Vilabu vingine vilivyobaki havina budi kuanzisha kitengo hiki na kuachana na masuala ya kamati za usajili ambazo zinaundwa na wajumbe wengi ambao hawana elimu katika suala la kusaka vipaji.
Viongozi wasiingilie mapendekezo ya benchi la ufundi; Timu karibia zote katika ligi ya Tanzania mabenchi yake ya ufundi hayana uhuru wa kimaamuzi na kimapendekezo, ipo ile kasumba ya viongozi kuingilia mambo ya usajili kwa lengo la kujipatia fedha, hii imekuwa ikiziumiza timu zetu na kuzifanya zipate wachezaji wadogo wenye viwango vidogo ambao hawaendani na ukubwa wa timu wanazosajiliwa na kupelekea kufeli.
Kutengwe bajeti kubwa ya usajili; Wachezaji wakubwa ni gharama, wachezaji wazuri na wenye vipaji vikubwa hawapatikani sokoni kirahisi kwani wanakuwa na ushindani, timu zetu hazina bajeti toshelevu ya usajili kiasi ya kuweza kusajili wachezaji wakubwa na hii inatokana na ukwasi mdogo wa vilabu vyetu na kuishia kupata wachezaji wadogo wa bei ndogo ambao huchangia kufeli.
Hivyo ushauri wangi kwa vilabu vyetu, watenge mafungu toshelevu juu ya usajili ili tupate sajili bora na sio bora sajili.
NB: KARIBU KWENYE ULIMWENGU WA KANDANDA