Dirisha dogo la usajili lilifungwa tarehe 31 mwezi uliopita na kushuhudia timu mbalimbali zikinunua na kuuza baadhi ya wachezaji.
Hawa ni baadhi ya wachezaji bora kusajiliwa na timu mbalimbali, na jinsi ambavyo watazisaidia timu zao katika mifumo tofauti.
Alexis Sanchez, Ametoka Arsenal na kujiunga katika timu ya Manchester United.
Msimu wa mwaka 2014/2015 alihusika kwenye 1/3 ya magoli ya Arsenal akifunga magoli 30 na kutoa pasi za mwisho za magoli 15 kwa msimu mzima.
Ana miaka mitatu akiwa katika nchi ya England hii ni moja ya faida kubwa kwa Manchester United. Wamebahatika kuchukua mchezaji ambaye siyo mgeni wa ligi kuu ya England.
Faida ya pili, Alexis Sanchez kihalisia ni mchezaji wa pembeni na Manchester United wamekuwa wakikosa mchezaji halisi wa pembeni hivo kuja kwake itakidhi mahitaji ya timu.
Faida ya tatu, Alexis Sanchez ana uwezo wa kucheza kama false 9, hivo anaweza kutumika kukidhi mahitaji ya timu kipindi ambacho haina Lukaku, pia Alexis Sanchez anauwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa pili( nyuma ya mshambuliaji wa kati).
Swali kubwa na zito ni kama Alexis Sanchez ataweza kuibeba vizuri jezi namba 7. Jezi yenye historia kubwa na klabu ya Manchester United ambapo iliwahi kuvaliwa na watu wazito kama Bryan Robson ( “Captain Marvel”), Eric Cantona, David Beckham , Cristiano Ronaldo. Tangia Ronaldo mwaka 2019 hakuna mtu ambaye amefanikiwa kufanya makubwa na jezi hii. Je Sanchez atafanikiwa?
Henrikh Mkhitaryan na Pierre- Emirick Aubameyang kwenda Arsenal. Wanakutana tena kwa mara nyingine katika timu ya Arsenal baada ya kuwahi kuwa pamoja katika timu ya Borrusia Dortmund
Swali kubwa kwa mashabiki wengi wa Arsenal namna ambavyo Arsene Wenger anaweza kuwatumia Laccazate , Ozil, Mkhitaryan na Aubameyang kwa pamoja.
Wote wanne wanaweza kucheza pamoja katika mifumo ifuatayo.
Mfumo wa kwanza ni mfumo wa 4-2-3-1 ambapo katikati watakaa Wilshere na Xhaka/Ramsey, mbele yao atakuwepo Mesut Ozil , pembeni kushoto atakuwepo Mkhitaryan na pembeni kulia atakuwepo Aubameyang na mshambuliaji wa mwisho atasimama Lacazzate.
Pia hata katika mfumo wa 4-4-2 Diamond pia unaweza ukawafanya wacheze pamoja huku mbele wakitumia washambuliaji wawili yani Laccazate na Aubameyang.
Msimu huu Aubameyang amefanikiwa kufunga jumla ya magoli 21 akiwa Borrusia Dortmund hivo anaenda kucheza na watu wanaojua kutengeneza nafasi za magoli kama Mkhitaryan na Ozil, hivo uwepo wake utaongeza nafasi ya ufungaji wa magoli katika timu ya Arsenal.
Lucas Moura Ametoka PSG kwenda Tottenham Hotspurs ,
ni usajili ambao haujaongelewa sana kwenye vyombo vya habari.
Ila ni usajili ambao utakuwa na matokeo makubwa ambayo yatazungumzwa sana kwenye vyombo vya habari. Lucas Moura anakuja kuongeza kasi katika eneo la mbele la Spurs, uzoefu wake wa kukaa kwenye timu kama PSG, kushiriki mara kwa mara kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya kutakuwa ni faida kubwa kwa Tottenham Hotspurs.
Theo Walcot Ametoka Arsenal kwenda Everton,
miaka 15 akiwa katika timu ya Arsenal na amefanikiwa kufunga magoli 100+ ikiwa ni wastani wa kufunga magoli 10 kwa kila msimu, uzoefu wake wa ligi kuu ya England ndicho kitu ambacho Everton wanaenda kunufaika nacho, pili ni mshambuliaji ambaye anaweza kutokea pembeni na akafunga au kutengeneza magoli.
Everton wamekuwa hawana wachezaji ambao wanauwezo wa kufunga wakitokea pembeni, pia Walcot ana uwezo wa kusimama kama mshambuliaji wa mwisho.
Van Djik Ametoka Southampton kwenda Liverpool.
Wamekuwa wakiteseka sana eneo la nyuma. Wanampata beki Van Djik ambaye anauwezo mzuri wa kukaba, pia anafaida kubwa hata kwenye kushambulia kwa kuanzisha mashambulizi kwenye timu na kufunga magoli kwa kutumia mashuti, mipira iliyokufa na mipira ya kichwa inayotokana na kona.
Giroud Ametoka Arsenal kwenda Chelsea.
Magoli 105 akiwa Arsenal ndani ya misimu mitano, wastani wa kufunga magoli 20 ndani ya msimu mmoja, anaweza akaonekana siyo mtu sahihi kwa Chelsea, ila kwa matumizi ya muda mfupi Chelsea wamepata kilichokizuri. Katika takwimu za msimu huu Chelsea ndiyo timu pekee iliyopiga krosi nyingi. Giroud ni moja ya watu wanaotumia vizuri Krosi kufunga. Anaweza kutumika katika mfumo wa 3-5-2 ambao unaonekana kutumiwa na Conte msimu huu. Ambao Mbele akakaa yeye na Morata , Morata akacheza kama mshambuliaji wa pili na Giroud akacheza kama mshambuliaji wa kwanza. Au katika mfumo wa 3-4-3 ambapo mbele wanakaa Giroud kama mshambuliaji wa kati, Morata na Hazard.
Aymeric Laporte Ametoka Athletico Bilbao kwenda Manchester City.
Usajili mzuri kwa Manchester City. Ni aina ya mabeki wanaoendana na aina ya uchezaji wa Pep Guardiola. Anaanzisha mashambulizi vizuri akiwa nyuma, timu zote za Pep Guardiola huanza kujenga mashambulizi nyuma. Pia kulikuwa na changamoto ya majeruhi katika eneo la mabeki wa nyuma hivo kumuongeza Laporte kutakuwa na msaada mkubwa kwa Manchester City katika kuongeza ukubwa wa kikosi.