Timu ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kutinga fainali katika msimu wa tatu wa kombe lá FA baada ya kupata ushindi katika uwanja wa Kambarage Shinyanga dhidi ya Stand UTD.
Tangu msimu huu wa Azamsports FederationCup uanze mechi zote za Mtibwa Sugar zimekua zikipangwa ugenini. Hivyo hakuna hata mchezo mmoja ambao Mtibwa amecheza Manungu complex mpaka kufika fainali itakayopigwa Arusha katika uwanja wa sheikh Amri Abeid.
Mtibwa Sugar imecheza michezo yake katika mikoa ya Iringa, Shinyanga na Dar es salaam na kufanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo yote hiyo ya ugenin.
Mechi Za Mtibwa Sugar Mpaka Fainali:
Majimaji Rangers 1 vs Mtibwa Sugar 2
Mtibwa Sugar ilianza kampeni zake za mwaka huu katika mashindano ya Azamsports FederationCup kwa kucheza na Mabingwa wa mkoa wa Iringa. Katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Ilulu Iringa Mtibwa ilipata ushindi wa mabao mawili kwa moja, huku magoli yote ya Mtibwa Sugar yakiwekwa kambani na Kelvin Sabato “Kiduku” huku lile la Majimaji likifungwa na Peter Michael kwa mkwaju wa Penalti.
Buseresere 0 Mtibwa Sugar 3
Katika hatua ya 16 bora Mtibwa Sugar walifanikiwa kupata ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi ya Buseresere ya Kahama. Magoli ya Mtibwa Sugar yaliwekwa kimiani na Hassan Dilunga, Ally Makalani na Haruna Chanongo.
AzamFc 0 vs Mtibwa Sugar 0 (8-9 PT).
Mchezo wa robo fainali uliopigwa katika dimba la Azam Complex ulizima ndoto za Azam za kushiriki michuano ya Kimataifa mwakani baada ya kupoteza mchezo huo kwa njia ya mikwaju ya penati baada ya kutoka suluhu katika dakika 90.
Katika mchezo huo Mtibwa walipata ushindi kwa kupata penati 9 huku Azam wakipata penati 8. Henry Joseph akikosa penati kwa upande wa Mtibwa Sugar huku Frank Dumayo na Abdallah Kheri wakikosa kwa upande wa Azam.
Stand UTD 0 vs Mtibwa Sugar 2
Mtibwa Sugar walikata tiketi ya kwenda Arusha kucheza fainali katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid baada ya kuifunga Stand UTD mabao mawili kwa bila.
Magoli ya Mtibwa Sugar yaliwekwa kambani na Hassan Dilunga katika kipindi cha kwaza.
Mpaka sasa Mtibwa Sugar wanasubiri kumjua mpinzani wao watakaecheza nae fainali kati ya Singida utd na JKT Tanzania katika nusu fainali ya pili itakayopigwa Jumatatu hii.