Sambaza....

Leo ligi kuu Tanzania bara inaendelea tena kwa michezo mbalimbali ambapo Alliance FC atakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa CCM Kirumba wakimkaribisha Mtibwa Sugar.

Mbeya City atakuwa katika uwanja wa Sokoine mjini Mbeya wakimkaribisha Coastal Union kutoka Tanga. Azam FC watakuwa Azam Complex kuwakaribisha Singida United.

Nicholaus Wadada raia wa Uganda akiitumikia Azam fc.

Watani wa jadi Simba na Yanga watakuwa kwenye viwanja viwili tofauti wakitupa karata zao kuelekea kwenye mechi yao ya Kariakoo Darby. Simba watakuwa Mtwara wakicheza na Ndanda FC huku Yanga wakiwa Mara wakicheza na Biashara United.

Yanga anaenda Mara huku akiwa na kumbukumbu nzuri ya kuchukua alama nne (4) za ugenini tangu likizo ya Corona iishe. Alishinda dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na akatoka sare dhidi ya JKT Tanzania pale Dodoma. Zifuatazo ni sababu kwanini leo Yanga anaweza kupoteza mchezo dhidi ya Biashara United.

Atupele Greeb akithibitiwa na Paul Ngalema

1: FAIDA YA UWANJA WA NYUMBANI.

Hii ndiyo faida kubwa ambayo Biashara United yuko nayo kuelekea mchezo huu, wako nyumbani tena kwenye uwanja ambao wamekuwa wakipata matokeo mazuri dhidi ya timu zinakuja kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume.

KMC FC walikuja kwenye uwanja wa nyumbani wa Biashara United mara baada ya likizo ya Corona kuisha na KMC FC walifungwa goli 4-0 na Biashara United.

Azam FC nao walipoenda kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma walitoka sare ya goli 1-1, kwa hiyo tangu likizo ya Corona iishe Biashara United wamekuwa na matokeo mazuri kwenye uwanja wao wa nyumbani kitu ambacho kitawapa morali kubwa wao kuelekea mchezo dhidi ya Yanga.

2: PRESHA YA MCHEZO WA WATANI WA JADI.

Kwa sasa Yanga wanaitazama mechi dhidi ya Simba ndiyo mechi muhimu iliyobakia kwa sababu mbili , sababu ya kwanza ni kwamba ni mechi ambayo ndiyo itaamua ushiriki wa Yanga kwenye michuano ya kimataifa kwa msimu ujao.

Kama watafanikiwa kuifunga Simba watatengeneza mazingira mazuri ya wao kwenda fainali ya kombe la Azam Federation Cup fainali ambayo itawapa nafasi kubwa ya wao kupata nafasi ya kushiriki kombe la Azam Federation Cup.

Sababu ya pili ni Yanga inaenda kukutana na Simba , Simba ambao ni watani wa jadi wa Yanga. Utani ambao unaifanya Yanga ifikirie zaidi umuhimu wa mechi ya Simba kuliko mechi zingine. Kwa hiyo kwenye mechi hii wanaweza wasiwekeze nguvu nyingi na akili zao kufikiria mechi ya Simba itakayochezea tarehe 12 mwezi huu.

3: BIASHARA YA KUTOSHUKA DARAJA.

Kwenye msimamo wa ligi kuu ya Tanzania bara , Biashara United yuko nafasi ya kumi, bado hana uhakika wa asilimia mia kuwa anaweza kubaki kwenye ligi kuu ya Tanzania bara au anaweza kuendelea kuwepo , ili kujitengenezea mazingira ya kujihakikishia abaki kwenye ligi kuu hii itamlazimu awekeze nguvu nyingi kwenye uwanja wake wa nyumbani ili kuhakikisha anapata alama hapa ndipo ugumu wa Yanga kushinda mechi hii unapoanzia

Sambaza....