Sambaza....

Leo mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania bara Yanga watakuwa kwenye uwanja wa Mkapa kucheza na Mbeya City katika mwendelezo wa ligi kuu Tanzania bara.

Yanga wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na kumbukumbu ya kupata sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu Tanzania bara.

Wakati huo Mbeya City wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa magoli 4 -1 na KMC FC kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi kuu. Leo wanakutana, nawapa nafasi kubwa Yanga kwa sababu zifuatazo ;

1: MATOKEO YA MECHI YA KWANZA.

Mechi ya kwanza dhidi ya Tanzania Prisons, Yanga ilikuwa na mategemeo makubwa ya kufanya vyema kutokana na usajili ambao waliufanya.

Lakini kwa bahati mbaya Yanga hawakufanya vyema. Kutokufanya kwao vyema kunawapa nafasi ya leo kuwaomba msamaha mashabiki wao kwa ushindi dhidi ya Mbeya City.

Matokeo ya mechi ya kwanza hayakuwa mazuri kutokana na kocha wao kuwa na muda mfupi na timu. Ameshakaa na timu wiki nzima tangu matokeo ya mechi ya kwanza.

Carlinho

Wiki hii imempa nafasi kubwa sana kwake yeye kujua angalau namna gani ambavyo anaweza kusahihisha makosa ya mechi iliyopita kwa sababu ameshakaa na wachezaji vyema.

2: UBOVU WA MBEYA CITY.

Mbeya City tangu msimu uliopita haikuwa imara sana. Ilinusurika kushuka daraja kwenye mechi ya mtoano. Ubovu wao unaonekana bado unaendelea , mechi yao ya kwanza wamefungwa magoli 4-1 dhidi ya KMC FC , hivo inaonekana bado kuna ubovu ndani ya kikosi cha Mbeya City kitu ambacho kitakuwa na faida kwa Yanga leo.

3: MATOKEO YA SIMBA

Moja ya kitu ambacho leo hii kitawapa nafasi kubwa Yanga kama msukumo wa kushinda mechi ni matokeo ya jana ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar .

Simba ilitoka sare, sare ambayo inawafanya kuwa na alama 4, hivo Yanga itapigana leo kuhakikisha wako katika mstari sawa na Simba ambao ndiyo wapinzani wao wakubwa.

4: HAMASA YA MASHABIKI WA YANGA

Baada ya sare dhidi ya Tanzania Prisons, Tulitegemea mashabiki wa Yanga watakuwa wamekufa moyo na timu yao lakini imekuwa tofauti.

Wiki hii Yanga imezindua jezi zake mpya . Mwitikio umekuwa mkubwa sana. Mwitikio ambao unaonesha bado mashabiki wana imani na Yanga hivo motisha bado iko juu.

Sambaza....