Leo hii wawakilishi wetu katika michuano ya kimataifa Yanga wataanza safari yao ya mechi za makundi ya shirikisho barani Afrika kwa kuanza kucheza na
USM Alger katika uwanja wa Stade Omar Hamadi nchini Algeria.
Maswali mengi ni namna gani ambavyo Yanga wataanza safari yao kufikia mafanikio makubwa katika michuano hii, ikiwa ni michuano pekee ambayo imebakiza kama michuano ambayo itaweza kumpa nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Mechi hii Yanga ana nafasi kubwa ya kupoteza kuliko kushinda kutokana na sababu zifuatazo.
1: Faida ya uwanja wa nyumbani kwa USM Alger. Moja ya sababu ambazo timu za ukanda wa Afrika Kaskazini kufanya vizuri katika michuano hii ni wao kutumia vizuri viwanja vyao vya nyumbani.
Leo hii USM Alger wako katika uwanja wao wa nyumbani, uwanja ambao katika mechi tano zilizopita walizocheza katika uwanja wao wa nyumbani hawajapoteza hata mechi moja, wakishinda mechi tatu na kutoka sare michezo miwili huku wakifunga magoli 12 na ƙkufungwa magoli 5.
Hii inatoa tafasri moja kuu, kwenye mechi za hivi karibuni za USM Alger kwenye uwanja wao wa nyumbani wamekuwa na timu ambayo ni ngumu kwao, pili wana wastani wa kufunga magoli 2 katika kila mechi ambayo wanacheza katika uwanja wao wa nyumbani.
Ukuta wao umeruhusu magoli 5 katika mechi mechi hizo tano ikiwa ni wastani wa kufungwa goli moja kila mechi.
Pamoja na kwamba wana wastani wa kufungwa goli moja kila mechi katika mechi tano zilizopita katika uwanja wao wa nyumbani lakini uhakikisha hawafungwi katika uwanja wao wa nyumbani.
2: Safu ya ushambuliaji ya USM Alger.
Hapo juu nimekuonesha safu yao ya ushambuliaji ilivyo kali katika uwanja wao wa nyumbani ambapo katika mechi tano zilizopita katika uwanja wao wa nyumbani wamefanikiwa kufunga magoli 12. Lakini ukiangalia katika mechi tano zilizopita ( walizocheza katika uwanja wao wa nyumbani na viwanja vya ugenini ) wamefanikiwa kufunga magoli 11 ikiwa ni wastani wa kufunga magoli 2 katika kila mechi.
Hii inaonesha kuwa wana safu ya ushambuliaji isiyo butu, ina uwezo wa kufunga goli katika kila mechi.
3: Historia ya USM Alger katika michuano ya CAF.
Katika viwango vya ubora vya muongo vilivyotolewa na shirikisho la mpira barani Afrika 2000-2010, USM Alger ilionekana ni timu ambayo inashika nafasi ya 18 katika viwango vya ubora wa vilabu barani Afrika.
USM Alger ilifanikiwa kufika fainali ya michuano hii ya shirikisho barani Afrika mwaka 2015 na kufungwa na TP Mazembe kwa magoli 4-1.
Hii inatosha kuonesha kuwa USM Alger ni timu ambayo ina historia ya kufanya vizuri katika michuano hii ya kombe la shirikishi barani Afrika.
4: Nafasi waliyopo kwenye ligi yao.
Wapo nafasi ya tano wakiwa na alama 42 . Nafasi hii haimpi nafasi ya yeye kufuzu kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.
Hivo wana hatiti ya kutopata nafasi ya kucheza michuano ya vilabu barani Afrika msimu ujao. Nguvu kubwa watawekeza huku ili kuhakikisha kuwa wanachukua kombe hili ili wapate nafasi ya moja kwa moja ya kushiriki tena michuano hii msimu ujao, na hii inawapa nguvu hasa wakiangalia kuwa waliwahi kufanikiwa kufika fainali ya michuano hii mwaka 2015.
5: Hali ya kikosi cha Yanga.
Yanga wamesafiri bila nyota wake muhimu ambao wameonekana kama nguzo imara katika timu hii msimu huu. Hawana Papy “Kabamba” Tshishimbi, Obrey “Chollo” Chirwa (Anaumwa Malaria), Kelvin “Patrick” Yondani (Majeruhi) na Ibrahim Ajib (Matatizo ya kifamilia).
Wachezaji wanne muhimu katika kikosi cha kwanza hawatokuwepo katika mechi hii. Kuwakosa wachezaji hawa nyota kwa Yanga itakuwa pigo kubwa na kwa USM Alger kutakuwa na wepesi katika mechi hii.