Klabu ya soka ya Fulham imeongeza nguvu kwenye kikosi chao kwa kumsajili winga wa zamani wa Liverpool Ryan Babel kutoka klabu ya Besiktas ya nchini Uturuki.
Babel mwenye umri wa miaka 32 ambaye aliwahi kudumu kwamiaka mitatu na nusu kwenye klabu ya Liverpool amejiunga na timu hiyo inayofanya vibaya hadi mwishoni mwa msimu huu.
Fulham inashika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi ikiwa alama tano kutoka katika mstari salama, na Babel amesema anaamini kabisa kuwa timu hiyo itasalia kwenye ligi “Nina uhakika kabisa na nina imani Fulham itasalia kwenye ligi, na hiyo ni moja ya sababu ya mimi kujiunga na timu hii,” amesema Babel ambaye msimu huu amefunga mabao sita akiwa na Besiktas.
Makamu mwenyekiti wa Fulham Tony Khan amesema “Ryan Babel anauwezo wa kucheza soka la kushambulia na ameonesha uwezo wake kwenye timu ya taifa na klabu, tunakaribisha uzoefu wake wakati ambapo tunatengeneza kikosi kwa ajili ya duru ya pili ya ligi,”
“Claudio na mimi tunaimani kubwa na Ryan, hasa anaporejea kwenye ligi kuu, tunajua atakuwa vizuri zaidi na kusaidia kikosi chetu,” ameongeza.
Baada ya kuondoka Liverpool mwaka 2007, Babel alijiunga na vilabu kama Hoffenheim ya Ujerumani, Ajax ya Uholanzi, Kasimpasa ya Uturuki, Al Ain ya Falme ya Kiarabu na Deportivo de La Coruna ya Uhispani kabla ya kuibukia Besiktas mwaka 2017.
Amecheza michezo 54 kwenye timu ya Taifa ya Uholanzi
akifunga mabao nane, pia aliwahi kuwa kwenye kikosi hicho kilichocheza mchezo
wa fainali na Uhispania katika kombe la dunia mwaka 2010.