Sambaza....

Klabu ya soka ya Ruvu Shooting itaendelea kuwakosa wachezaji wao 16 kuelekea mchezo kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania dhidi ya Mbeya City siku ya Jumatano kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Wachezaji nane kati hao 16 ni wale wa kikosi cha kwanza ambao wameachwa kabisa mkoani Pwani kutokana na kuwa na Majeraha akiwemo Abdalah Rashid, Isa Kanduru, Fuluzulu Maganga na Zuberi Dabi, huku wengine nane wakizuiwa kucheza kutokana na kukosa leseni.

Msemaji wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema jambo la wachezaji ambao hawana leseni linashughulikiwa na pengine wakapatiwa leseni hizo kabla ya mchezo wa Jumatano na kuruhusiwa kucheza.

Tunao wachezaji wanane wa kikosi cha kwanza walikuwa ni majeruhi ambao tuliwaacha kabisa Mlandizi, lakini kuna wengine wanane ambao walizuia kucheza kwenye mchezo uliopita, na ndio jambo ambalo limenileta jijini Dar es Salaam kuja kushughulikia hilo na lililobakia ni TFF kuwaingia kwenye system na kutupatia leseni hizo ili wacheze.” Masau amesema.

Ikumbukwe wachezaji wanane wa Ruvu Shooting walizuiwa kucheza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons ambao uliisha kwa sare ya mabao 2-2 kutokana na kukosa leseni.

Aidha kuelekea kwenye mchezo wa Jumatano dhidi ya Mbeya City Masau amesema kikosi chini ya kocha Abdulmatik Haji kinaendelea kujiandaa na kwamba mashabiki wa timu hiyo jijini Mbeya wameipa nafasi kubwa Ruvu Shooting kuibuka na ushindi.

Mpaka sasa Ruvu Shooting wameshacheza michezo mitatu wakitoka sare michezo miwili na kufungwa mchezo mmoja matokeo ambayo yanawafanya kufikisha alama mbili na kushika nafasi ya 18 kati ya timu 20 zinashoriki ligi kuu kwa msimu wa 2018/2019.

Sambaza....