Ligi ya Saudia Pro League inaweza kuwa “ligi ya tano bora duniani” ikiwa itafanikiwa kuvutia wachezaji wenye majina makubwa, anasema mshambuliaji wa Ureno Cristiano Ronaldo.
Lionel Messi, Karim Benzema na Luka Modric wamehusishwa na kuhamia Saudi Arabia na Ronaldo, 38, anasema “wanakaribishwa sana” kuungana naye.
Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or amemaliza msimu wake wa kwanza akiwa na Al Nassr baada ya kujiunga mwezi Desemba.
Ana mkataba hadi 2025 na akaongeza “ataendelea hapa” msimu ujao.
Paris St-Germain wamethibitisha kuwa Messi ataondoka katika klabu hiyo msimu huu wa joto na mshambuliaji huyo wa Argentina, 35, ana jukumu la kuwa balozi wa utalii wa Saudi Arabia.
Wachezaji-wenza wa Ronaldo wa zamani wa Real Madrid, Benzema na Modric pia wanafikiriwa kutafuta uhamisho mzuri mwisho wa maisha yao ya soka.
“Kama wanakuja, wachezaji wakubwa na wenye majina makubwa, wachezaji wachanga, ‘wachezaji wazee’, wanakaribishwa sana kwa sababu hilo likitokea, ligi itaimarika kidogo,” Ronaldo alisema kwenye mahojiano na SPL.
“Ligi ni nzuri sana lakini nadhani tuna nafasi nyingi za kukua, ligi ina ushindani, tuna timu nzuri sana, wachezaji wazuri sana wa Kiarabu.
“Lakini wanahitaji kuboresha zaidi miundombinu. Hata uamuzi, mfumo wa VAR, unapaswa kuwa wa haraka zaidi.”
Chanzo BBC.