Timu zote zilikuwa zinacheza mfumo wa 4-4-2 lakini kwenye maumbo ya mifumo ndiyo zilikuwa zinatofautiana.
Real Madrid ilikuwa inacheza 4-4-2 Diamond na Juventus ilikuwa inacheza 4-4-2 katika umbo la flat?
Upi uimara na udhaifu katika mifumo hii kwenye mechi ya jana?
Massimiliano Allegri alionekana kuzidiwa kwenye mbinu na Zinedine Zidane kutoka na aina ya mfumo wa 4-4-2 flat alioamua kuutumia katika mechi hii.
Kwanini nasema hivi? Juventus iliwalazimu kuwatumia Santos na Costa pembeni mwa uwanja na katikati kubaki na Rodrigo Bentancur pamoja na Sami Khedira, Paolo Dyabala alikuwa anashuka chini katikati kuwasaidia kina Rodrigo Bentancur na Sami Khedira, mbele alibaki Gonzalo Higuan ambapo kulikuwepo na mabeki wawili wa kati ( Sergio Ramos na Varane) hii iliwasaidia Real Madrid kuwa na beki mmoja wa kati kusogea mpaka katikati ya uwanja , na beki mwingine kubaki na Higuan.
Eneo la katikati mwa uwanja likawa na watu wengi wa Real Madrid kuliko wa Juventus kwa sababu Real Madrid walikuwa wanacheza 4-4-2 Diamond ambayo iliwawezesha kina Isco kuingia eneo la katikati muda mwingi huku wakitokea pembeni wakati timu ikiwa na mpira, hivo kufanya timu iwe na viungo watatu wa katikati dhidi ya viungo wawili wa katikati.
Hii iliongeza uzito wa mashambulizi kwa RealMadrid ambapo pembeni waliwatumia mabeki wao wa pembeni kushambulia.
Juventus tuliwazoea wakiwa na watu watano kipindi ambapo timu inapokuwa haina mpira (inapokuwa inajizuia), lakini jana ilikuwa na watu wanne hali ambayo ilisababisha wao watengeneze uwazi eneo la pembeni, uwazi ambao ulisababisha goli la kwanza na la pili kupatikana kwa sababu mpira ulipita eneo la pembeni mwa uwanja.
Hiki ndicho kiliwasaidia sana RealMadrid , mfumo wa 4-4-2 Diamond kwao kuliwafanya wawe na watu wengi eneo la katikati na wachezaji wengi kuhusika katika kushambulia.
Wakati Juventus mfumo wa 4-4-2 flat ulikuwa hauna faida kubwa kwao kwa sababu walikuwa na watu wachache eneo la katikati na wakati wanajizuia walikuwa wanatengeneza uwazi eneo la pembeni mwa uwanja.
Massimiliano Allegri angerudi kwenye mfumo wake wa 3-5-2?
Hii ingekuwa na tija kubwa sana kwake kiulinzi kwa sababu angekuwa na watu wengi katika eneo la nyuma, hali ambayo isingesababisha yeye atengeneze uwazi eneo la pembeni nyuma, uwazi ambao ulitumika kupatikana kwa goli la kwanza na la pili.
Isco ameendeleza kile alichokifanya dhidi ya Argentina?
Hakufunga goli, lakini alikuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha RealMadrid. Alikuwa analeta uwiano mzuri katika eneo la kiungo cha kushambulia na eneo la ushambuliaji.
Kwanini nasema hivo? Isco alikuwa anashuka eneo la katikati kuchukua mipira, na kuwafanya kina Toni na Modric kuwa wanachukua mipira kwa Casemiro kisha kumpa Isco.
Isco alikuwa anawalisha kina Ronaldo na Benzema bila wao kuhangaika kushuka chini kutafuta mipira.
Pia alivyokuwa anakokota mipira, ilikuwa inawasaidia RealMadrid kupata uwazi wa kupitishia mipira na kina Modric na Kroos walikuwa wanatumia uwazi huo kupokea mipira na kutoa pasi au kupiga mashuti ndiyo maana tuliona mashuti ya Toni Kroos mawili yakigonga mwamba