Sambaza....

Mabingwa wa soka kutoka nchini Rwanda wameungana na USM Alger kufuzu katika robo fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuwachapa Dar Young Africans kwa bao 1-0 katika mchezo wa mwisho wa kundi D la michuano hiyo.

Rayon ambao waliingia katika mchezo huo wakiwa na uhitaji mkubwa wa alama tatu, walifanikiwa kupata bao la pekee na la ushindi kupitia kwa Bonfilscaleb Bimenyimana katika dakika ya 19 baada ya kuwapiga chenga walinzi wa Yanga kabla ya kuachia shuti kali lililopita pembeni mwa kipa Beno Kakolanya na kujaa wavuni.

Licha ya Yanga kujaribu kutafuta bao la kusawazisha kwa kushambulia kwa kushtukiza kupitia kwa Deus Kaseke na Heriter Makambo lakini safu ya Ulinzi ya Rayon ilikuwa imara kuzuia hatari zote katika mchezo huo ambao umepigwa kwenye uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda.

Kwa ushindi huo Rayon Sports wameshika nafasi ya pili katika kundi D nyuma ya USM Alger ambao nao wameichapa Gor Mahia kwa mabao 2-1 waliokuwa na nafasi ya kufuzu katika hatua ya robo fainali kutoka katika kundi hilo.

Vikosi vilivyocheza.

Rayon: Bashunga, Mugabo, Rutanga, Rwatubyaye, Ange, Nyandwi, Muhire, Donkor, Manishimwe, Mugisha, Bimenyimana (Mugume 79′).

Young Africans: Kakolanya, Yondani, Michael, Chikupe, Shaibu (Ngonyani 61′), Kaseke, Simon, Loth, Migomba, Buswita, Makambo (Mhilu 68′).

Sambaza....