Shirikisho la soka Afrika, CAF leo limetoa ratiba ya mechi za hatua ya awali za mashindano ya klabu bingwa Afrika na Shirikisho.
Ratiba hiyo inaonyesha mechi za awali zitachezwa kuanzia tarehe 9-11 mwezi wa nane, huku za marudiano ni kuanzia tarehe 27-29 mwezi wa nane mwaka huu kwa mashindano yote ya shirikisho na klabu bingwa Afrika.
Kwa upande wa Simba wataanzia ugenini kupepetana na UD do Songo ya Nchini Msumbiji wakati majirani zao Young Africans wataanzia nyumbani kucheza na Township Rollers ya Botswana mechi hizi zote zinatarajiwa kupigwa kati ya tarehe 9-11 mwezi Agosti.
Kwa upande wa Shirikisho Afrika, KMC na Azam Wote waanzia ugenini, KMC atacheza na AS Kigali ya Rwanda ya Haruna Niyonzima wakati Azam watacheza na Ethiopia 1 ya nchini Ethiopia mechi hizi pia zinatarajiwa kuchezwa tarehe sawa na mechi za klabu bingwa Afrika.
Ratiba hii huenda ikawa mwiba kwa klabu ya Simba ambayo hutumia vema tarehe 8 mwezi Agosti kupitia tukio lake la kihistoria la Simba day. Tukio ambalo hutumika kuwatambulisha wachezaji wapya, kutambulisha uzi mpya na kuziuza, pia huwakutanisha wanamsimbazi wote katika eneo moja na kupata burudani.
Tukio hili limefanikiwa kwa miaka 9 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 na aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo Mzee Hassani Dalali.
Maadhimisho ya miaka 10 ya Siku ya Simba huenda yakaingia dosari kuendana na ratiba ya klabu bingwa Afrika, yaani kama Simba itatakiwa kucheza tarehe 9 nchini Msumbaiji maana yake timu itakikiwa kusafiri tarehe 6 au 7 kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo ambao ni muhimu kwa Malengo ya Simba.
Dua za Simba kwa sasa, ni CAF kuamua samba acheze tarehe 11 ili Simba day iweze kwenda kama ilivyopangwa, lakini hata hivyo kuna njia mbadala inaweza kutumika ikiwemo kusogeza mbele ratiba ya tukio hilo japo itapoteza ladha kwani wachezaji watakuwa wameshaonekana kupitia mechi hiyo ya klabu bingwa Afrika.