Sambaza....

Kufuatia tetesi za muda mrefu kumhusu kocha wao Nasraddine Nabi kuachana na klabu hiyo sasa klabu ya Yanga imetoa taarifa rasmi kuachana na Mtunisia huyo.

Nabi 58 amekua akihusishwa na kutimkia Afrika kusini na taarifa rasmi ya klabu inasema “Uongozi wa Yanga unapenda kuutarifu umma umefikia makubaliano ya kuachana na kocha wake Nasradinne Nabi baada ya kocha huyo kuomba kutokuongeza mkataba mpya,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza “Mkataba wa Yanga na Nabi unamalizika mwishoni mwa msimu huu.”

Kufuatia mafanikio makubwa waliyoyapata Yanga wakiwa chini ya Kocha Nabi wakitwaa makombe mawili ya FA, mawili ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii mara mbili amejitambulisha Afrika na kuwa lulu kwa klabu vigogo barani Afrika.

Nasraddine Nabi akiwa na mashabiki wa Yanga.

Yanga hawakua na budi zaidi ya kumshukuru Mtunisia huyo aliyekuja kuvunja utawala wa Simba waliobeba ubingwa wa Ligi mara nne mfululizo.

“Uongozi wa Yanga Sports Club unamshukuru kocha Nasraddine Nabi kwa kipindi chote alichofanya kazi katika klabu yetu na tunamtakia kila lakheri katika safari yake mpya,” ilimalizia taarifa hiyo.

Tayari Yanga imeshaanza mchakato wa kutafuta kocha mpya atakaerithi mikoba ya Mtunisia huyo ambae wiki hii huenda akatambulishwa Kaizer Chiefs.

Sambaza....