Sambaza....

Klabu ya soka ya Al Hilal ya Sudan kupitia ukurasa wao wa Facebook, imethibitisha kumnasa mshambuliaji wa Tanzania Thomas Ulimwengu ambaye hakuwa na timu kwa kipindi kirefu sasa toka avunje mkataba na AFC Eskilstuna ya Sweden kutokana na kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara.

Al Hilal wamesema kuwa mchezaji huyo alitua jana mjini Khartoum kumalizana nao ili aweze kuisaidia timu hiyo ambayo inaongoza kundi A la ligi kuu ya Sudan wakiwa na alama 30 pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo ipo kundi B pamoja na timu za Al Masry, UD Songo na RS Berkane.

“Amewasili jioni katika uwanja wa ndege wa Khartoum, lengo la klabu ni kuona anaungana nasi, na anajulikana kuwa ni miongoni mwa washambuliaji bora Afrika kutokana na kasi yake anapokuwa katika eneo hatari,” Taarifa ya klabu hiyo imeeleza.

Ulimwengu anarejea Afrika kwa mara nyingine baada ya kuondoka TP Mazembe mwaka 2016 akiisaidia timu hiyo kutwaa mataji kadhaa likiwemo taji la klabu Bingwa Afrika akiwa na Mtanzania mwenzake Mbwana Samatta.

Akiwa TP Mazembe toka mwaka 2011 hadi 2016 Ulimwengu alifanikiwa kufunga mabao 33 katika michezo 122 aliyocheza klabuni hapo.

Sambaza....