Mshambuliaji wa timu ya soka ya Azam FC Donald Ngoma huenda akaonekana kwa mara ya kwanza kunako michuano ya ligi kuu soka Tanzania Bara pale timu yake itakapokuwa ikipepetana na Lipuli FC siku ya Ijumaa.
Ngoma ambaye amekuwa na mejaraha ya muda mrefu, ambayo yalimfanya kuvunja mkataba na Yanga na kujiunga na Azam ameanza kufanya mazoezi na kikosi cha timu kubwa baada ya siku kadhaa kuwapo katika mazoezi na kikosi cha timu ya vijana.
Afisa habari wa Azam Jaffary Idd Maganga amesema mpaka sasa wanamatumaini makubwa kwa mchezaji huyo kucheza katika mchezo ujao, hata hivyo itategemea na kiwango chake atakachokionesha katika mazoezi.
“Kucheza kwa Ngoma au kutocheza kutategemea na kiwango chake kwenye mazoezi na pia jinsi gani anavyorudi taratibu taratibu uwanjani,” Maganga amesema.
Kwa upande wa Mohamed Yakubu ambaye naye amekuwa katika kipindi kirefu cha majeraha toka mwezi Februari mwaka huu, ameanza mazoezi na wenzake lakini yeye hana asilimia kubwa ya kucheza katika mchezo huo wa Ijumaa.
Maganga amesema Yakubu hawezi kucheza kwa sababu ndo kwanza ameanza mazoezi pengine mchezo baada ya ule dhidi ya Lipuli, “Yakubu ameanza mazoezi na wenzie leo yeye atakuwa bado kurejea uwanjani kwa sababu toka mwezi Februari hajagusa mpira wala kuingia uwanjani,”.
Azam ambao wamerejea jijini Dar es Salaam wakitokea mikoa ya Kanda ya Ziwa, watajitupa uwanjani siku ya Ijumaa kucheza na Lipuli mchezo ambao awali ulipangwa kufanyika siku ya Alhamis kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mpaka sasa Azam FC wapo katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 11 baada ya kushuka dimbani mara 5, wakizidiwa alama mbili na vinara Mbao FC ya jijini Mwanza wenye alama 13.