Sambaza....

Rais wa Klabu ya Real Betis, Angel Haro, amesema anaamini klabu hiyo ni miongoni mwa klabu zinazokuwa kwa haraka na kwamba wameshaanza kutambua nafasi yao kama klabu inakua kwa kasi.

Angel Haro ameyasema hayo baada ya klabu hiyo maarufu kama Los Verdiblancos kuwafunga Sevilla bao 1-0 kupitia kwa Joaquin Sanchez katika mchezo wa ligi uliofanyika Jumapili na kuwafanya timu hiyo kufikisha alama nne katika mechi tatu ambazo wamecheza.

“Betis inakuwa kwa kasi hivi sasa, tunamatumaini makubwa huko mbele, na tunafuraha kwa namna mambo yanavyokwenda, lengo letu ni kuwa klabu inayokuwa, ni kitu kizuri kuona kabla ya kuingia kwenye wiki ya FIFA tumewafunga wapinzani wetu, ni ushindi ambao kwa wakati wote huwafanya mashabiki wa Betis kuwa na furaha,” Haro amesema.

“Utofauti wa klabu hizi mbili (Betis na Sevilla) sio mkubwa sana kwa sasa, hapo zamani kidogo Sevilla waliweza kusajili vizuri na kutupa wakati mgumu, sasa tunataka kufikia mafanikio ambayo Sevilla wamekuwa nayo kwenye uwanja kama vilabu vingine vingi vya Laliga vilivyoweza,” Haro ameongeza.

Katika mechi za ligi kuu Hispania, Real Betis walianza kwa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Levante kabla ya kutoka sare ya 0-0 na Deportivo Alaves na baadae kuwafunga Sevilla kwa bao 1-0.

Msimu uliopita Real Betis walimaliza katika nafasi ya 6 kwa kukusanya alama 60 nafasi ambayo iliwapa nafasi ya kushiriki michuano ya Europa League.

Sambaza....