Sambaza....

Vyombo vya uchunguzi nchini Ufaransa vimeanza uchunguzi kwa klabu ya Paris Saint Germain iwapo kulikuwa na upangaji wa matokeo katika mchezo dhidi ya Red Star Belgrade katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Taarifa kutoka nchini Ufaransa zinasema kuwa katika mchezo huo ambapo PSG walishinda kwa mabao 6-1 kulikuwa na viashiria vya upangaji wa matokeo, kwani maofisa wa klabu ya Red Star wanasadikika kubashiri mchezo huo kwa kuweka kiasi cha Euros Milioni 5 kuwa timu yao ingepoteza kwa mabao zaidi ya matano.

Gazeti la L’Equipe la nchini Ufaransa limeandika kuwa ofisi ya Mwendesha mashtaka ya nchini Ufaransa (PNF) ilitaarifiwa kuhusu tukio hilo na shirikisho la soka Barani Ulaya (UEFA) ili kuanza kuchunguza suala hilo.

Aidha vilabu vyote viwili vimekana kuhusika na tukio hilo.

“FC Red Star kwa hasira kubwa na kwa kuchukizwa tunakana taarifa hizi, taarifa ya gazeti hilo inaweza kudhuru na kuharibu taswira ya klabu na ndio maana tunaiomba UEFA na wachunguzi kutoka Serbia na Ufaransa kuchunguza kwa makini na kupata ukweli wa jambo,” Taarifa ya klabu ya Red Star ya nchini Serbia imesema.

“Kwa sasa teknolojia na mambo mengine yamekuwa, na ndio maana itakuwa si rahisi kuliacha suala hili bila kupata ukweli, Red Star inatarajia kupata ukweli kwa kipindi kifupi na kuondoa mashaka yetu ya kuhusika na jambo hili,” imesema.

Kwa upande wao PSG taarifa yake imesema kuwa “Kwa mshangao na chukizo tunasikitika kusema kuwa klabu hii imebaki kuheshimu mchezo wa soka, kwa maana ya ushindani wa kweli kwa hiyo tunakana kuhusika kwa namna yoyote na suala hilo,”.

Katika mchezo huo uliopigwa Oktoba 3, mabao matatu ya Neymar pamoja na Edinson Cavani, Angel Di Maria na Kylian Mbappe yaliweza kuipa ushindi PSG wa mabao 6-1  huku Mjerumani Marko Marin akifunga bao la kufutia machozi kwa Red Star.

Ikumbukwe mpaka sasa PSG wapo nafasi ya tatu kwenye kundi C la ligi ya Mabingwa barani Ulaya wakiwa nyuma ya Liverpool licha ya kuwa na pointi tatu kila mmoja katika michezo miwili na Red Star wakishika mkia, na Napoli akiongoza kwa alama nne.

Sambaza....