Sambaza....

Mlinda mlango mkongwe wa Juventus na timu ya Taifa ya Italia Gianluigi Buffon amehusishwa na kujiunga na klabu ya soka ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari za michezo wa Sky ni kuwa Kipa huyo mwenye umri wa miaka 40 baada ya kuondoka Juventus anaweza kujiunga na miamba hiyo ya soka nchini Ufaransa na tayari mazungumzo yameanza.

Rais wa klabu ya PSG Nasser Al-Khelaif kwa siku za hivi karibuni amekuwa akimwagia sifa lukuki kipa huyo hata alipohojiwa na gazeti la L’Equipe la nchini Ufaransa alikiri kutamani kuwa na kipa huyo lakini alisema kuwa kipa Alphonse Areola ataendelea kuwa chaguo la kwanza la kocha Thomas Tuchel.

Al-Khelaifi

“Tuna Areola, yeye ni chaguo letu la kwanza, na nadhani itakuwa hivyo hata msimu ujao, Buffon ni kipa mzuri, ana karama na ni mtu mzuri, najua kila timu inatamani kuwa naye,” Al-Khelaif alisema.

Jumamosi iliyopita Buffon aliagwa kwa heshima katika mchezo wake wa mwisho kuitumikia Juventus, wakishinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Hellas Verona.

Buffon ambaye alijiunga na Juventus akitoke Parma ameichezea timu hiyo michezo 656 katika miaka yake 17 klabuni hapo, hivyo kama atajiunga na PSG utakuwa ni usajili wa kushtukiza kwani tayari watu walidhani ya kuwa hatocheza tena soka la ushindani.

Sambaza....