Uongozi wa klabu ya soka ya Tanzania Prisons umetoa Baraka zote kwa mshambuliaji Mohamed Issa Rashid kujiunga na mabingwa wa Tanzania Bara Simba Sports Club, huku wakimlalamikia Eliuter Mpepo ambaye ameondoka bila kuaga.
Katibu mkuu wa Tanzania Prisons Havintishi Abdallah ameeleza kuwa Mohamed Rashid aliuomba kuondoka na kutaja wapi anapoelekea na kwa kuwa hawana desturi ya kuwazuia wachezaji wao wakamruhusu kuondoka tena tayari wameshampatia na barua.
“Sisi ndio tulimruhusu Mohamed Rashid, baada ya kutaka kumuongezea kwenye mkataba yeye akasema anataka kwenda kupata changamoto nyingine, sasa sisi Prisons hatuna kawaida ya kumzuia mchezaji na tayari tumeshampa barua, na tunajua anaelekea Simba ametuambia,” Havintishi amesema.
Kwa upande wa Eliuter, katibu huyo wa klabu hiyo ambayo inamilikiwa na jeshi la Magereza mkoani Mbeya amesema yeye imekuwa tofauti kwani ameondoka klabu lakini hayajaaga wala kuwaambia anaelekea wapi.
“Si huyo tu ambaye ameondoka kuna Eliuter Mpepo, sijui kapata timu gani sijui Singida Sijui Yanga, hajawa muwazi kwetu kama mwenzake ambaye alisema anakwenda Simba,” Havintishi amesema.
Vilevile Havintishi amesema mapengo hayo yatazibwa kwani wamekuwa na utaratibu mzuri wa usajili na ndiyo kitu ambacho kinawaumiza kichwa kwa sasa ili kufanya usajili wa maana na kuendelea kutesa kunako ligi kuu soka Tanzania.