Sambaza....

Wawakilishi wa nchi na kanda ya Afrika Mashariki katika ligi ya klabu bingwa Afrika, Simba SC tayari wameshawasili nchini Algeria kwa ajili ya kucheza mchezo wao wa 5 katika hatua ya makundi.

Hadi sasa msimamo wa kundi D unaonyesha kuwa Simba wana alama 6 nafasi ya pili, nyuma ya Al ahly yenye alama 7, huku Js Saoura akiwa na alama 5 katika nafasi ya tatu, na mkia ukiburuzwa na AS Club Vita ikiwa na alama 4.

Kikosi kilichosafiri kina wachezaji 20 ambao ni Aishi Manula, Deo Munish, Zana Coulibaly, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Mohammed Hussein, Paschal Wawa, Paul Bukaba, James Kotei, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Clatus Chama, Rashid Juma, Haruna Niyonzima, Abdul Suleiman, John Bocco, Mohammed Ibrahim, Meddie Kagere na Adam Salamba.

Kikosi hiki kinamkosa Emmanuel Okwi na Juuko Mursheed wote  kutoka kikosi cha kwanza. Waganda hao wanakosekana kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo idadi ya kadi za njano na majeraha.

Kukosekana kwao huenda kukawa pengo kubwa kwa wekundu wa Msimbazi wanaohitaji matokeo japo sare kwa udi na uvumba ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali.

Kiufundi, pengo la Okwi ni kubwa kuzidi la Juuko, hii ni kwa sababu, Simba haina mchezaji sampuli ya Okwi. Hapa namaanisha uwezo binafsi, kujituma uwanjani, kutimiza majukumu na maagizo kutoka kwa kocha, na kubadilika kulingana na hali ya mchezo bila kuagizwa na kocha.

Pengo la Juuko ni kubwa lakini ni rahisi kuzibika. Kuziba pengo hilo kunahitaji utimamu wa mwili na akili wa Paul Bukaba na Paschal Wawa. Bukaba ni mtu wa kazi kama Juuko wote mapungufu yao ni kukosa utulivu wanapokuwa na mpira, na hii huwatofautisha wao na Wawa.

Kwa mantiki hiyo, pengo la Okwi litazibika lakini kimkakati. Ni mbinu pekee ndizo zitakazoziba pengo la Okwi.Pengo la Okwi na Juuko ni lazima lizibwe ili Simba ishinde au kupata sare.

Kwanini Okwi ni pengo?

Jibu la swali hilo ni kukurudisha nyuma hadi kwenye mechi dhidi ya Al- ahly, na Yanga, Dar es Salaam. Okwi ni pengo, tena kubwa. Nakutolea mfano mechi hizi  mbili kwa sababu ndio zilikuwa mechi kubwa, na Simba ilihitaji matokeo, na imeyapata.

Dhidi ya Al-Ahly, Simba ilianza kwa kumiliki mpira ndani ya dakika kama 20 za kipindi cha kwanza, baadae wakagundua kuwa, Al-Alhy walikuwa wanawaachia wamiliki mpira, kikubwa wasiwadhuru. Baada ya Aussems kung’amua hilo haraka akabadili “game plan”.

Simba ikaanza kupiga mipira mirefu, ikitoka kwa Wawa au Juuko mpaka kwa Okwi aliyekuwa anacheza namba 7. Okwi alitumika kama mpokea mipira, na kuanzisha mashambulizi kwa kukimbia kwa kasi kuelekea eneo la hatari.

Muda huo kipindi anafanya hayo yote, anawapa nafasi washambuliaji wa kati, Kagere na Bocco kukaa maeneo sahihi kwa ajili ya kupokea mpira wa mwisho kutoka kwa Okwi na kufunga au kutengeneza nafasi.

Aina hii ya uchezaji iliwafanya Al- Alhy wasishambulie kupitia pembeni kwa beki wake namba 3, Alli Maaloul ambaye alibanwa vizuri na Okwi.

Jukumu kama hili pia, alilifanya katika mechi dhidi ya Yanga. Okwi alihama upande wa kulia alikokuwa Gadiel Michael na kumfuata Paulo Godfrey aliyeonekana kushambulia kupitia kulia. Okwi pia alifanikiwa kumzima Paulo, na badala yake Paulo akawa anamchezea rafu Okwi.

Kwahiyo Okwi hutumika kuzima mashambulizi ya timu pinzani kupitia pembeni. Uwepo wake na uhatari wake unawafanya mabeki washindwe kupandisha timu na kuanzisha mashambulizi.

Tumeona kwanini Okwi ni pengo, sasa acha tulizibe pengo lenyewe, maana Simba inahitaji ushindi au sare. Pengo linazibika lakini kwa masharti ambayo yanahitaji mwalimu kuwa na msimamo thabiti juu ya kile anachokiamini.

Mfumo.

Simba imekuwa ikitumia mfumo wa 4-4-2 unaobadilika badilika hadi 4-5-1 kwa mechi za ugenini. Na katika mfumo huo Simba wakala 5, kwa kila mechi. timu zote zilizowafunga zina aina moja ya soka, tofauti ni ndogo sana.

Al-Ahly na AS Club Vita wote hucheza mpira wa haraka, kwenda mbele. Ahly hutumia pasi ndefu na fupi, huku AS Club Vita hutumia mipira mirefu, hii ni kutokana na aina ya washambuliaji waliokuwa nao, kuwa na kasi.

JS Saoura hutumia mfumo wa 4-2-3-1 wakiwa nyumbani. Mechi mbili walizocheza nyumbani wamepata alama 4, zote ni kupitia mfumo huo. JS Saoura hujaza viungo wengi katikati na hushambulia kupitia katikati (central-attacking).

Aina hii ya mfumo dawa yake ni kutanua uwanja, yaani Simba lazima waingie na mfumo wa  “4-4-2 diamond”. Eneo la kiungo litawaliwe na wanaojua kukaba na kupiga pasi. Kiungo wa chini anaweza kuwa James Kotei, viungo wa kati wanaweza kuwa Jonas Mkude na Mzamiru Yassin au Hassan Dilunga, na kiungo mshambuliaji anaweza kuwa Clatus Chama. Vyovyote watakavyoanza lakini lazima wawe wanapitia pembeni ili kuitanua safu ya kiungo ya Saoura na  kupata nafasi ya kucheza.

Game plan.

Game plan za Aussems kwa mechi za ugenini ndio huwa zinawaadhibu Simba. Ugenini ni ugenini tu, timu lazima iwe na nidhamu kwa timu mwenyeji. Katika mechi mbili za ugenini Simba ilikuwa ikiingia uwanjani ikitumia silaha ya kumiliki mpira. Silaha iliyowagharimu kwa kiasi kikubwa.

Simba lazima kwanza waingie na game plan ya kupiga mipira mirefu na kushambulia kwa kasi. Yaani mpira uchukue sekunde chache kutoka kwa safu ya ulinzi kwenda kwa washambuliaji. Mabeki wa pembeni ni lazima wawe wepesi kushambulia na kulinda kwa wakati mmoja.

Licha ya kumkosa Okwi ambaye ndiye angekuwa mchezaji sahihi katika mfumo huu, lakini Bocco anaweza kufanya hivyo pia. Kwahiyo Simba wasiende kumiliki mpira bali waende kuliandama lango la Soura kwa kufikisha mipira katika eneo lao la hatari muda wote.

Kiujumla sio lazima kumiliki mpira, unaweza ukawaachia wamiliki mpira, lakini hakikisha umiliki huo hauwapi nafasi ya kukudhuru. Man U walishinda mbele ya PSG ugenini, waliwaheshimu, waliwaachia umiliki wa mpira lakini wao walishambulia kwa kasi na kushtukiza, kisha wakazitumia nafasi chache walizozitengeneza na kupata ushindi wa 3-1.

Majukumu mapya kwa Bocco.

Ukiwatazama Bocco na Kagere, anayefaa kuwa Straika wa mwisho ni Kagere. Hii ni kwa sababu Kagere ana uwezo wa kukaa eneo moja tofauti na Bocco. Na hivyo ndivyo Okwi huwa pia. Yaani Okwi naBocco wanafanana kimikimbio isipokuwa Okwi hucheza kama winga na Bocco kama straika.

Bocco atakuwa na kazi kubwa zaidi, kwani “game plan” itamtaka amzunguuke Kagere, yaani acheze kushoto na kulia kwa Kagere, ahakikishe anamlisha mipira ya kufunga.

Bocco

Bocco pia lazima awe na uwezo wa kuusoma mchezo mapema, ajue unahitaji nini na yeye afanye nini. Lazima atimize jukumu la kukaba kuanzia juu, na kuzima eneo la ushambuliaji kupitia kwa mabeki wa pembeni. Kama beki wakulia wa Soura ndio hatari basi yeye acheze 11, na kama ni beki wa kushoto basi yeye akacheze 7.hivi ndivyo Okwi huwa anafanya.

Nidhamu ya mchezo.

Hiki ni kitu kipana sana katika soka. Wachezaji wanatakiwa wawe na nidhamu kwa kila tendo uwanjani. Kuanzia ukabaji, game plan, pasi, aina ya pasi, lugha, saikolojia,  hamasa, matumizi ya nafasi, uharaka na ufanyaji wa maamuzi.

Mkude

Simba wanahitaji kucheza kwa nidhamu kubwa sana, hasa “marking”, na aina ya mchezo wanaotaka kuucheza. Ni kama tendo la kisaikolojia tayari limeshajijenga akilini mwa wachezaji kuwa mechi ya ugenini ni ngumu kupata matokeo. Huku nikukosa nidhamu ya mchezo.

Timu iundwe vizuri kisaikolojia, akili zao lazima zikubali kupambana ili kupata matokeo, kisha kila mchezaji awe tayari kutoa kile alichonacho kwa moyo wake wote na kujituma kwa kufa na kupona.


Sambaza....