Sambaza....

Yanga imecheza mechi mbili mpaka sasa hivi baada ya kurejea ligi kuu ya Tanzania bara , mechi ambazo wamefanikiwa kupata alama nne na wamepoteza alama mbili mpaka sasa hivi. Kitu ambacho siyo kibaya .

Mechi zote ni za ugenini , tena kwenye viwanja ambavyo siyo vizuri lakini wamefanikiwa kupata alama nne ndani ya michezo miwili . Kwenye mechi zote mbili ambazo wamecheza hawakuwa na wachezaji na wawili muhimu wa kikosi chao.

Papy Kabamba Tshishimbi pamoja na Bernard Morrison hawakuwepo kwenye kikosi cha Yanga kilichokuwepo Shinyanga kwenye mechi dhidi ya Mwadui FC na kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania pale jijini Dodoma.

Mechi zote mbili walifanikiwa kufunga goli, ambapo kwenye mechi dhidi ya Mwadui FC walishinda kwa goli moja kwa sifuri huku kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania walitoka sare ya goli moja kwa moja.

Pamoja na kufanikiwa kutofungwa mechi hizi mbili ila kuna mapengo makubwa mawili ambayo yameonekana kwa kiasi kikubwa ndani ya kikosi cha Yanga , Yanga hawakuwa na Papy Kabamba Tshishimbi pamoja na Bernard Morrison.

Swali kubwa hapa ni yupi ambaye alihitajika zaidi kwenye kikosi cha Yanga kwenye hizo mechi mbili walizocheza ? Tuanze kumtazama mchezaji mmoja baada ya mwingine.

Nafasi ya Bernard Morrison alicheza Balama Mapinduzi , ambaye hakucheza kama mchezaji halisi wa pembeni kama ambavyo Bernard Morrison huwa anacheza , Balama Mapinduzi alikuwa Anatolia pembeni mwa uwanja na kuingia katikati ya uwanja.

Kila alipokuwa anaingia katikati ya uwanja alikuwa anaongeza nguvu katika eneo la kati ya uwanja huku pembeni kukiwa na udhaifu . Mfano goli la JKT Tanzania lililofungwa na beki wa kulia wa JKT Tanzania, Maiko Aidan.

Maiko alifanikiwa kufunga goli lile baada ya kupanda mbele huku akiwa huru zaidi na kupiga shuti ambalo liliingia moja kwa moja , wakati anapiga mpira Balama Mapinduzi hakuwepo eneo la pembeni mwa uwanja kusaidia kukaba.

Balama Mapinduzi alikuwa ameruhusu eneo la pembeni mwa uwanja kuwa na uwazi , kitu ambacho siyo rahisi kuonekana kwa Bernard Morrison ambaye muda mwingi huwa anakaa pembeni mwa uwanja na mabeki wengi wa kulia huwa wanakuwa na hofu ya kupanda mara kwa mara kutokana na madhara yake.

Benard Morisson.

Huu ndiyo ulikuwa umuhimu wa Bernard Morrison , lakini eneo ambalo Yanga walihitaji nguvu zaidi ni eneo la kiungo cha kati . Eneo ambalo lilikuwa linaifanya timu isisogee kwenda mbele kwa kiasi kikubwa.

Kelvin Yondani alicheza kama kiungo wa kuzuia , kitu ambacho alikifanya vyema kwa upande wa kuzuia. Alikuwa na uwezo wa kuizuia safu ya ulinzi ya Yanga vizuri lakini kulikuwa na kitu kimoja ambacho hakuwa na uwezo wa kukifanya , nacho ni kupandisha timu.

Yondani akiwahi mpira kuuzuia..

Alikuwa anazuia vyema lakini lilipokuja suala la yeye kupiga pasi za kuanzisha mashambulizi lilikuwa suala ambalo hakulifanya is ufanisi mkubwa , lilipokuja suala la yeye kukokota mipira kwa kwenda mbele lilikuwa suala ambalo hakulifanya kwa ufanisi mkubwa.

Hii ilikuwa inawalazimu wachezaji wa eneo la kiungo cha mbele kushuka chini kwa ajili ya kuchukua mipira badala ya kusubiri mipira . Kushuka kwao chini kuliwafanya wapunguze idadi ya wachezaji katika eneo la mbele hali ambayo ilisababisha Yanga kutopata ushindi kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania.

Papy Kabamba Tshishimbi.

Hapa ndipo umuhimu wa Papy Kabamba Tshishimbi unapokuja, inawezekana Bernard Morrison ni mchezaji hatari lakini Papy Kabamba Tshishimbi ndiye mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga na alihitajika zaidi hasa kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania.

Kuna sababu tatu ambazo zinambeba kwenye hili, moja ana uwezo wa kuanzisha mashambulizi kwa kupiga pasi za kwenda mbele kwa ufasaha. Ana uwezo wa kukokota mipira kwa kwenda mbele na ana uwezo wa kufunga kwa kutokea katikati ya uwanja.

Sambaza....