Kocha wa klabu ya Simba ametema cheche kuelekea mchezo wa “Derby” kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Pablo Franco amezungumzia mchezo huo akisema mechi dhidi ya Yanga ni mchezo mkubwa lakini wao ni wazuri zaidi kuliko wapinzani wao.
“Ni mechi kubwa (dhidi ya Yanga) mbele yetu, tumetoka kucheza mchezo wa robo fainali dhidi ya Orlando na kila mmoja wetu aliona kilichotokea katika mchezo ule.” Pablo Franco akizungumza mbele ya waandishi.
“Sisi tumezoea kucheza mechi kubwa kama hizi nadhani mliona wenyewe katika mchezo wa robo fainali. Na ndio maana nasema sisi timu kubwa na nzuri kuliko wenzetu.” Pablo Franco
Kocha Pablo pia alisema wenzao wana faida ya kupumzika mda mrefu na kutokucheza mchezo mgumu kama ambavyo wao ratiba imewabana.
“Tunakwenda kucheza na timu ambayo ilikua imepumzika kwasababu hawakua na mchezo wa Kimataifa, lakini tupo tayari tumejiandaa kupata alama tatu.” Aliongeza Pablo Franco
Nae mlinzi wa kulia wa Simba Shomary Kapombe amesema wao kama wachezaji wamejiandaa vizuri kueleka mchezo huo na watawafuta machozi mashabiki wao baada ya kutolewa katika michuano ya Kimataifa.
“Tumejiandaa vyema katika mchezo huu, ni mchezo mkubwa na wenye hisia kubwa kwa watu wote.” Kapombe alisema
“Tumejiandaa kucheza vizuri na kutoa burudani kwa mashabiki wetu. Tumetolewa michuano ya CAF sisi kama wachezaji tumekaa na tukaongea huu ndio mchezo mkubwa na wenye hisia kubwa hivyo mchezo dhidi ya Yanga tutautumia kuwarejesha mashabiki katika hali ya kawaida.” Shomary Kapombe.