Sambaza....

Kikosi cha wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club kimeondoka leo asubuhi kikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Morogoro ambapo watacheza mchezo wa ligi dhidi ya Mbao FC kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Humo.

Meneja wa timu hiyo Patrick Rweymamu amesema wachezaji wote waliosafiri leo asubuhi wapo katika hali nzuri na kwamba wanatarajia leo jioni watafanya mazoezi ya kwanza kabla ya mchezo huo ambapo unatarajiwa kufanyika Jumapili.

Amesema wanakwenda na imani yao ni kuwa maandalizi waliyoyafanya yatawasaidia kufanya vizuri katika mchezo huo mgumu kwani Mbao ni miongoni mwa timu ambazo zimewapa wakati mgumu.

“Wachezaji wote ambao tumeondoka nao wapo kamili na hakuna matatizo yoyote kwa mpaka muda huu, tunategemea kufika Morogoro asubuhi hii, tufanye mazoezi leo jioni na kesho tujiandae vizuri kwa ajili ya mtanange wetu dhidi ya Mbao FC,

“Tunawaheshimu Mbao, katika msimu uliopita walitupa changamoto na msimu huu nadhani katika mchezo wa kwanza hatukupata matokeo mazuri, kwa hiyo ni imani yetu katika maandalizi tuliyoyafanya tunaenda kufanya vizuri katika mchezo huu wa Jumapili,” ameongeza.

Simba wanashuka dimbani dhidi ya Mbao wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao katika duru ya kwanza kwa bao 1-0, mchezo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mpaka sasa Simba wana alama 54 katika nafasi ya tatu baada ya kushuka dimbani mara 21 wakati Mbao ambao watakuwa na benchi jipya la ufundi katika mchezo huo litakaloongozwa na Shaban Mayanga na kusaidiwa na Fulgence Novatus wapo nafasi ya 14 wakiwa na alama 36 baada ya kucheza michezo 30.

Sambaza....