Kipa wa Mamelodi Sundowns Denis Onyango amejibu swali la iwapo anafikiria kustaafu soka la kulipwa hivi karibuni. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alishinda taji la 10 la ligi kuu nchini Afrika Kusini kufuatia ushindi wa Sundowns msimu huu.
Denis Onyango alishinda mataji saba akiwa na Masandawana na matatu akiwa na SuperSport United na kumfanya kuwa mchezaji aliye na mataji mengi zaidi ya ligi nchini Afrika Kusini maarufu kama PSL.
Kuwasili kwa Ronwen Williams msimu huu katika klabu ya Sundowns pia kumemfanya mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Uganda kuwa mlinda mlango namba mbili mbele ya kipa namba moja Bafana Bafana.
Onyango aliulizwa wakati wa mahojiano na kituo cha Redio cha SABC PhalaPhala FM siku ya Alhamisi ikiwa alikuwa akifikiria kustaafu “Bado nataka kunyanyua mataji haya,” Onyango alisema kwenye kipindi cha michezo cha ‘Zwamitambo na kuongeza “Mwili bado unasema naweza, labda msimu mmoja au miwili zaidi huwezi kujua. Lakini kwa sasa klabu inasema bado unaweza kutupa kitu.
“Nadhani klabu pia inategemea uzoefu wangu na uongozi ambao ninajaribu kuleta kwenye chumba cha kubadilishia nguo. Kwa hivyo ndio mwili bado unaniruhusu kucheza kwa muda mrefu kidogo. kwa nini isiwe hivyo?
Onyango aliongeza kuwa si yeye tuu bali kuna wachezaji wengi wanacheza wakiwa na miaka 40 na zaidi lakini pia kwake yeye anaiskiliza klabu yake kama bado wataendelea kumpa nafasi.
“Nimeona wachezaji wengine wakicheza hadi wakawa 40 au 42. Lakini tutaona klabu inafikiria nini kunihusu lakini pia lazima nisikilize mwili wangu,” alimalizia Onyango.