Sambaza....

Klabu ya soka ya Manchester United imemtangaza kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya umeneja toka kuondoka kwa Jose Mourihno kuwa meneja wa kudumu kwa mkataba wa miaka mitatu.

Kocha huyo ambaye alikuwa akiifundisha Molde ya nchini Norway toka mwaka 2015 amechukua rasmi mikoba ya Jose Mourihno katika kikosi hicho baada ya kuiwezesha Manchester United kufanya vizuri toka kustaafu kwa Sir Alex Ferguson.

“Toka siku ya kwanza nimefika hapa niliona hapa ni nyumbani kwangu, ni heshima kwangu kuichezea Manchester United, lakini pia kuanza kazi yangu ya ukocha hapa, kwa miezi michache iliyopita imekuwa ni sehemu nzuri ya maisha yangu, nataka kuwashukuru makocha wenzangu, wachezaji na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri ambayo tayari tumeianza, hii ni kazi ambayo muda wote nimekuwa nikiiwaza kuifanya ni imani yangu tutaendelea kuiletea mafanikio ambayo mashabiki wetu wanapaswa kuyaona,” amesema Solskjaer baada ya kutangazwa.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu hiyo akifunga mabao 126 katika michezo 366 kati ya mwaka 1996 na 2007 anakuwa kocha wanne tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson, huku watangulizi wake David Moyes, Louis Van Gaal na Jose Mourihno wakishindwa kabisa kuvaa viatu vya Ferguson.

Alianzia kazi ya ukocha akiwa Manchester United kama kocha wa timu ya akiba mwaka 2010 kabla ya kwenda kuifundisha Molde ya Norway mwaka 2011 hadi 2014 kabla ya kupewa kazi nzito ya kuinusuru Cardiff City ishuke daraja mwaka 2014 na mwaka mmoja baadae akarejea tena Molde hadi alipojiunga na Manchester United kama kocha wa muda Disemba mwaka jana.

“Tangu amekuwa hapa mwaka jana, matokeo yanazungumza yenyewe, ni zaidi ya kiwango kizuri na matokeo mazuri, Ole ameleta kitu kikubwa kwenye klabu hii kama mchezaji na kocha pia, amewapa wachezaji chipukizi nafasi ya kuonesha uwezo wao na anauelewa mkubwa wa tamaduni za klabu hii inamaanisha kwamba ni mtu sahihi kwa ajili ya klabu hii,” amesema Mtendaji mkuu wa klabu Ed Woodward.

Toka amefika Manchester United mwaka jana, ameiongoza timu hiyo katika michezo 19 akishinda michezo 14, na ameiongoza kupata alama nyingi zaidi kwa kipindi hicho kuliko timu yoyote ile inayoshiriki ligi ya England.

Sambaza....