BAADA ya kuanza msimu kwa mwendo wa chini, mfungaji bora wa ligi kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Mganda, Emmanuel Okwi ameanza kuwasha moto wake mwezi huu baada ya kufunga magoli saba- ikiwemo ´HatTrick´ katika michezo mitatu iliyopita ya Simba SC.
Okwi ilimlazimu kusubiri hadi mchezo wa mzunguko wa saba kufunga goli lake la kwanza mapema mwezi huu Simba walipoichapa African Lyon magoli 2-1, akafunga tena goli lingine moja wakati walipoichapa Stand United.
Haitoshi, Okwi akafunga mara mbili katika ushindi wa Simba 5-1 Alliance School Jumatano iliyopita na jana Jumapili akafunga HatTrick yake ya kwanza msimu huu wakati alipoiongoza Simba kuwaangamiza Ruvu Shooting 5-0 na hivyo kumfanya mshambulizi huyo wa timu ya Taifa ya Uganda kufikisha magoli saba- akilingana na kiongozi wa muda mrefu katika chati ya wafungaji, Ambokile Eliud wa Mbeya City FC.
MAGOLI 20+…
Kwa kasi aliyoonyesha Oktoba hii- kufunga jumla ya magoli saba katika michezo minne, Okwi bila shaka anaweza kufunga tena magoli 20 kama alivyofanya msimu uliopita ama zaidi ya hayo.
Ndio, alifunga magoli manne peke yake katika ushindi wa 7-0 dhidi ya Shooting msimu uliopita lakini magoli yake matatu dhidi ya timu hiyo ya Pwani jana Jumapili yameonyesha straika huyo bado ana hamasa kubwa ya kutaka kufanya vizuri zaidi na makali yake hayo yakiendelea bila shaka atatetea tuzo yake hiyo binafsi ya ufungaji bora.
Okwi amekuwa kwenye kiwango kizuri kiufungaji mwezi huu. Ukiachana na magoli yake saba aliyoyafunga katika michezo minne ya ligi kuu Tanzania Bara, Oktoba 10 na 16 mwaka huu alifunga pia magoli mawili katika michezo miwili ya Uganda kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika- CAN2019.