Sambaza....

Msimu jana ulikuwa mgumu sana kwa Yanga kuanzia ndani mpaka nje ya uwanja. Ilikuwa Yanga ambayo ilikuwa na matatizo mengi sana. Matatizo ambayo yalichangia kwa kiasi kikubwa wao kupoteza ubingwa wao kwa wapinzani wao Simba.

Haikuwa Yanga ile ambayo tulikuwa tumeizoea, Yanga ambayo ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa mara ya tatu mfululizo. Yanga ambayo ilikuwa inashinda sana tena kwa magoli mengi sana kwa sababu ya kuwa na washambuliaji ambao walikuwa wanaonekana ni washambuliaji hatari sana.

Ilikuwa ngumu kutoka salama katika mikono ya Yanga, kwa sababu kulikuwa na asilimia kubwa ya wewe kuadhibiwa kila unapokutana nao. Tena walikuwa wanatoa adhabu kubwa haswaa. Hawakuwa na huruma kabisa, ilikuwa Yanga ambayo ilikuwa imebeba washambuliaji wenye njaa, Yanga ambayo ilikuwa imebeba watu wakatili sana eneo la mbele, watu ambao walikuwa wanaogopeka sana.

Watu ambao walizifanya timu pinzani zisione sehemu ya kutokea kila zinapokanyaga miguu yao kukutana na Yanga. Kulikuwa na asilimia kubwa ya wao kufungwa tu.

Na hii ni kwa sababu Yanga ilikuwa imesheni watu wenye roho ya kikatili katika eneo la mbele, watu ambao walihakikisha Yanga ionekane Yanga bora, Yanga ambayo ilikuwa na ushindani wa hali ya juu.

Ilikuwa ngumu kukwepa kipigo kutoka kwao, kuna wakati Donald “Ndombo” Ngoma alipokuwa anakukosa kwa mguu wake wa kulia, Amis Tambwe anakuadhibu kwa kichwa chake cha kikatili.

Simon Msuva akikukosa kwa shuti lake Kali, Obrey Chirwa anakuangamiza kwa pigo laini tu la ndani ya eneo la kumi na nane. Hivo ndivo maisha yalivyokuwa yanaendelea katika timu ya Yanga.

Walikuwa na uhakika wa kula na kusaza, tena chakula chenye mboga saba wakisindikizwa na muziki mzuri uliokuwa unakifanya chakula chao kiteremke taratibu tumboni mwao.

Hali hii ni tofauti sana kwa sasa!, Yanga hawali tena wakashiba vizuri. Idadi za mboga pale mezani zimepungua. Hakuna tena mboga saba kwenye meza yao. Chakula chao ni chakuunga unga, hawana tena watafutaji wenye hasira ya maisha. Wana watu ambao wamekuja kumalizia uzee wao pale!, wazee ambao ujana wao walikuwa watafutaji haswaaa, lakini muda wao umeshapita.

Hakuna asiyejua utafutaji uliokuwa unafanywa na Mrisho Ngassa kipindi chake. Muda huu tunamlazimisha kuwa mtafutaji wakati ni muda wake wa kutulia na kupumzika ili ale alichokuwa anakitafuta enzi za ujana.

Chirwa (Kushoto) na Hans (Kulia), kocha wa Azam FC sasa. Hapa ni wakati wote wakiwa Yanga.

Hata yule Amis Tambwe aliyekuwa anaunda kamati ya mauaji akiwa na kina Obrey Chirwa, Donald “Dombo” Ngoma na Simon Msuva, siyo Amis Tambwe wa kipindi hicho. Kabadilika sana, majeruhi yamekuja kupora ubora wake, hawezi kuisaidia sana Yanga kama kipindi kile alipokuwa msaada mkubwa.

Kwa sasa macho ya wana Yanga yamebaki kwa Mcongo , Makambo. Mtu ambaye siyo hatari sana. Wa kawaida sana, na kinachosikitisha ni kwamba ukawaida wake upo sehemu ambayo siyo ya kawaida.

Sehemu ambayo haiitaji watu wa kawaida kusimama kama watetezi wa timu hiyo. Lakini yeye ndiye kasimama. Hata watu ambao wanakaa benchi kama mbadala wake hawana uwezo mkubwa wa kuifanya Yanga iogopeke kama kipindi kile ambacho kina Amis Tambwe walikuwa wametengeneza kamati ya mauaji.

Dirisha hili dogo wanahitaji sana kuongeza mtu ambaye atawasaidia sana, mtu ambaye ni mtafutaji. Nilipomuona Chirwa akiwa na viongozi wa Yanga wakitazama mechi ya Yanga katika uwanja wa Taifa nilijua Yanga wanataka kufanya naye mazungumzo ya kurudi katika timu.

Kitu hiki kilikuwa kitu cha muhimu sana kwa sababu kwa kipindi hiki Yanga wanamwihitaji sana Obrey Chirwa kuliko Obrey Chirwa anavyoihitaji Yanga.

Huyu ndiye aliyeibeba Yanga msimu uliopita, msimu ambao ulikuwa na changamoto nyingi sana kwa klabu ya Yanga. Hali mbaya ya uchumi ambayo ilipunguza sana morali ndani ya timu. Majeruhi ya wachezaji muhimu hasa hasa eneo la mbele.

Donald Ngoma alimaliza msimu akiwa anauguza majeraha, Amis Tambwe alimaliza msimu akiwa anauguza majeraha pia. Akawa amebaki Obrey Chirwa tu kama alivyo Makambo kwa sasa.

Obrey Chirwa aliwabeba Yanga sana. Alifunga sana. Kitu ambacho kwa sasa Yanga ndicho wanakikosa, hawafungi sana. Na wanahitaji mtu ambaye anaweza kufunga sana. Na Obrey Chirwa walikuwa mtu sahihi na kitu kizuri ni mchezaji ambaye asingepata kuingia ndani ya timu kwa sababu anajua mazingira yote ya Yanga.

Sambaza....