Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini Phil Masinga amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 49 akiwa anapatiwa matibabu kwenye hospitali ya Parktown mjini Johannesburg.
Rais wa shirikisho la soka nchini Afrika Kusini Danny Jordan amethibitisha kifo hicho na kusema family ya soka imepoteza miongoni mwa watu waliokuwa na uwezo akiwa ndani na nje ya uwanja.
“Ni siku ya huzuni kwa familia ya kandanda hapa Afrika Kusini, imepoteza mtu aliyejitolea kwa ajili ya kandanda, ndani na nje ya uwanja,” Taarifa ya Jordan imesema.
Masinga alipelekwa hospitalini hapo mwezi Disemba mwaka jana kwa ajili ya matibabu hadi mauti yalipomkuta leo asubuhi, anakumbukwa kwa kufunga bao ambalo liliisaidia Afrika Kusini kufuzu kwa mara ya kwanza michuano ya kombe la dunia mwaka 1998.
Ameichezea timu ya Bafana Bafana michezo 58 akifunga mabao 8, pia amewahi kuichezea Leeds ya nchini Uingereza mwaka 1994 na 1996 akifunga mabao matano, vilabu vingine ambavyo Masinga amevitumikia ni pamoja na Jomo Cosmos, Mamelod Sundowns na Bari ya nchini Italia.