Sambaza....

Bado siku sita tu kufika tarehe 12 ya mwezi July, siku ambayo itakua ni nusu fainali ya mchezo wa Azam Sports Federation Cup (Kombe la FA) kati ya vilabu vikubwa nchini na Afrika Mashariki na Kati, Simba na Yanga.

Simba na Yanga wanakwenda kukutana katika mchezo wa nusu fainali ambapo kabla ya kufika hapo wote walishinda michezo yao ya robo fainali iliyopigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaa. Simba iliifunga Azam bao mbili bila huku Yanga wao walimtoa Kagera kwa mabao mawili kwa moja.

Mchezo huu wa FA utatusaidia kutupa majibu ya maswali tuliyobaki baki nayo baada ya michezo miwili ya Ligi Kuu kuisha na Yanga kuibuka na alama nne kati ya sita. Mchezo wa kwanza uliisha kwa sare ya mabao mawili kwa mawili na wapili Yanga walishinda bao moja sifuri.  Miongoni mwa maswali tuliyobaki nayo ambayo tutajibiwa July 12 ni haya:

Luis Miquissone alithibitiwa na wachezaji wa Yanga.

1. Yanga wanaijulia Simba?

Mchezo wa kwanza Simba aliongoza kwa mabao mawili ya Meddie na Kanda lakini iliwachukua dakika 5 tu kwa Balama na Mo Banka kusawazisha na mchezo kuisha kwa sare. Lakini mchezo wa pili Benard Morisson aliipa ushindi Yanga kwa kiki kali ya mpira wa adhabu.

Katika michezo yote hii miwili Simba waliingia uwanjani wakipewa nafasi kubwa ya kuibuka washindi. Lakini Yanga kwa mara zote wameweza kucheza vizuri na kuibuka na alama nne. July 12 itatupa majibu kama ni kweli Yanga wana mbinu nzuri za kiufundi za kuweza kuizuia Simba licha ya kusheheni nyota kibao.

Luc Aymael kocha mkuu wa Yanga sc.

2. Yanga wana mbinu nzuri katika michezo ya mtoano?

Yanga inasifika kucheza mchezo wa kupata matokeo huku wakiwa na mbinu nzuri za kuweza kuamua mchezo. Licha ya kutocheza mchezo wa kuvutia sana lakini Yanga imekua na uwezo mkubwa wa mbinu linapokuja swala la matokeo (Rejea mchezo wa robo fainali wake dhidi ya Kagera).

Hata katika mchezo wa mwisho dhidi ya Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao moja huku wakiweza kucheza kwa kuzuia kwa kipindi cha pili chote na kushambulia kwa kushtukiza.

3. Simba imekua kibonde wa Yanga msimu huu?

Licha ya kusheheni nyota wenye ubora wa hali ya juu wa nje na ndani ya nchi na pia kunyakua ubingwa wakiwa na michezo sita mkononi lakini msimu huu wameshindwa kufua dafu mbele ya Watani zao Yanga. Tayari wamepoteza mchezo mmoja na sare moja msimu huu.

Hivyo wamebakiwa na mchezo mmoja wa nusu fainali ya FA wa kuweza kufuta uteja mbele ya Yanga ama kuhalalisha uteja katika msimu huu.

Sven Vandebroeck.

4. Sven kupewa mkono wa kwaheri Simba?

Sven ndie kocha aliepoteza rekodi ya Mnyama mbele ya Yanga yakutopoteza mchezo kwa misimu mitatu mfululizo baada ya kichapo cha bao moja bila katika mchezo wa raundi ya pili. Lakini pia zipo za chinichini kocha huyo hawavutii maboss wengi wa Msimbazi kutokana na matatizo yake binafsi lakini pia uwezo wa uchezaji wa timu.

Endapo atapoteza mchezo tena dhidi ya Yanga huenda ikakoleza safari yake yakutimuliwa na Simba na kuache rekodi mbovu miongoni mwa makocha waliopita Simba mbele ya Yanga.

Sambaza....