Sambaza....

Mpira ni sayansi , yaani lazima kuwe na utaratibu maalumu ambao utaiwezesha timu kupata matokeo kutokana na hitaji la mechi husika.

Simba Sc kwa mara nyingine wanatupa karata yao nyingine katika michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kumtandika Mbabane Swallows ya eSwatini kwa jumla ya magoli 8-1 na kuwafanya wasonge mbele na kukutana na Nkana Red  Devils ya Zambia.

Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na uchu wa kusonga mbele, kutokana na uwekezaji mkubwa wa timu kwa ujumla. Chini ya kocha Mbelgiji Patrick Aussem, Simba ina malengo ya kuvuka hatua hii ya mtoano na kuingia hatua ya makundi na hatimaye kusonga mbele zaidi.

Ukiitazama Simba na kisha ukaitazama Nkana utabaini mambo mengi ambayo  ni tofauti kwa timu zote mbili. Nkana ni timu nzuri, ina historia kubwa barani Afrika, na hata nchini Zambia. Kikosi cha Nkana kinatumia mfumo wa kushambulia pembeni kupitia mabeki wa pembeni na viungo wa kati na wa pembeni, kupiga pasi ndefu kuelekea kwa mawinga na kisha mawinga hao kukimbia na mpira kuelekea langoni au kupiga krosi.

Nkana kama timu ina kikosi cha wachezaji 29 wakiwa na wastani wa umri wa miaka 27, hii ina maana kuwa, umri wa wachezaji wengi wa timu hiyo ni wakubwa nah ii inaleta dhana nzima ya uzoefu katika kikosi hicho cha Nkana. Mchezaji hatari zaidi katika kikosi hicho Walter Bwalya, mwenye miaka 23, anatumia mguu wa kushoto na hupenda kupitia pembeni yaani kulia na kushoto.

Wacheazji wengi wa Nkana wanaonekana kuwa na vipaji vikubwa hasa kukaa na mpira na kupiga pasi ndefu. Hivyo mpira wa Nkana huwa hauchezewi sana katikati bali huchezewa pembeni mwa  uwanja, kupitia kwa mabeki wa pembeni na viungo pamoja na washambuliaji.

Kutokana na aina ya uchezaji wa Nkana bila shaka Simba ina nafasi kubwa ya kuwa muamuzi wa mchezo. Kwanini nasema hivi? Ni ukweli kuwa Simba ina kikosi kizuri kuwazidi Nkana katika kila idara. Safu ya kiungo ya Simba ndio muhimili wa kikosi kizima cha Simba kwa sasa. Chini ya Mkude Jonas, Clatus Chama, James Kotei ndio Simba huwa inatuliza mzuka wa timu pinzani na kuifanya iendelee kuhaha kutengeneza nafasi.

Mpira wa kisasa, timu hutengenezea mashambulizi kutokea kwa goli kipa, kwenda kwa viungo ambao mara nyingi huwa ni wapishi kwa washambuliaji na wakati mwingine wanaweza wakafunga na ndio maana Chama hadi sasa hivi ana magoli 3 katika mashindano haya.

Katika michezo miwili dhidi ya Mbabane, Simba ilicheza kwa staili tofauti ikiwa nyumbani na hata ugenini lakini matokeo ya ugenini ndio yaliyokuwa natija kubwa na mafanikio makubwa na hata soka lilichezwa vizuri. Katika mechi ya awali iliyochezwa nyumbani katika uwanja wa taifa, Jonasi mkude alicheza kama kiungo mshambuliaji, James Kotei akiwa kama kiungo wa chini, huku Clatus Chama akicheza kama kiungo huru anayeweza kupitia sehemu ya kulia au kushoto, na Simba ilishinda goli 4-1 lakini hadi dakika ya 82 Simba 2-1, hii ina maanisha kuwa mfumo huu wa kumpandisha Mkude juu eti awe anakabia kuanzia juu haukuleta mafanikio makubwa ukilinganisha na mchezo wa pili ambapo , Mkude na Kotei wote walikuwa viungo wa chini huku Emmanuel Okwi na Clatus Chama wakicheza juu, yaani Okwi kushoto na Chama kama kiungo mshambuliaji, na Simba ilifanikiwa kuilaza 4-0 Mbabane.

Katika mechi ya leo nakumbuka Jose Mourinho anaposema kikosi cha ushindi huwa hakibadilishwi bila shaka Aussem ataanza na mfumo alioutumia kuiua Mbabane Swallows katika mchezo wa ugenini.

Kiufundi wanasema, ukitaka kujilinda, lazima ushambulie. Ni mechi ya ugenini bila shaka Simba watahitaji kumiliki mpira, na kushambulia maana kiasili Simba ni timu ya kumiliki mpira na kutengeneza nafasi ya kufunga magoli. Katika mechi ya leo, Simba haitotegemea kutumia upande wa mabeki wa pembeni kushambulia kwa kuwa Nkana kiasili wanashambulia kupitia pembeni kwahiyo mabeki wa pembeni kama Tshabalala hawatokuwa na uwezo wa kupanda na kushambulia.

Natarajia kuona Simba ikipitia katikati kuliko pembeni, hivyo bila shaka kocha Aussem atajaza viungo katikati na kumuacha Meddie Kagere na John Boko kuwa washambuliaji wa kati na wa mwisho. Emmanuel Okwi anatokea pembeni katika upande ambao mchezaji hatari wa Nkana, Walter Bwalya atakaocheza hii ina maana kuwa, Okwi atakuwa na uwezo wa kurudi kumsaidia beki wa pembeni kama ambavyo huwa anafanya katika mechi za ligi kuu Tanzania Bara.

Mfumo watakaoutumia lazima ubadilike kutokana na aina ya uchezaji wa mpinzani lakini naamini, Nkana wataingia kwenye mechi hii wakiwa na nidhamu na tahadhari kubwa kwani Simba kwa sasa ina safu kali ya ushambuliaji  na  viungo wenye weledi mkubwa wa kukaba na kupiga pasi za mwisho akiwemo Chama, Hassan Dilunga, Mkude, Kotei na Shiza Kichuya.

Nategemea kumuona Erasto Nyoni akicheza pembeni, beki ya kulia kwa kuwa huko ndiko kuna udhaifu mkubwa. Nyoni kucheza pembeni kutaleta faida kubwa hasa katika kushambulia na hata kupiga pasi ndefu. Nyoni ni mzuri katika ukabaji na tukumbuke Nkana wanapitia pembeni kwahiyo Simba inahitaji mabeki wa pembeni wenye uwezo mkubwa wa kukaba na kumiliki mpira. Kama atacheza Nicolas Gyan huenda Nkana wakatumia nafasi hiyo kutengeneza mashambulizi kupitia upande wake.

Pia sio mbaya kama Aussem ataamua kumuacha mshambuliaji mmoja nje kati ya Boko na Kagere na kumuingiza kiungo mmoja mwenye uwezo wa kukaba kuanzia juu, kumiliki mpira na kupiga mashuti, naye ni Kichuya, kama atakuwa katika kiwango chake bila shaka ataleta tija kwa timu yake.

Mabadiliko makubwa na yenye tija nayaona hasa katika idara ya ulinzi, Juuko Murshid ana nafasi katika gemu ya leo, Erasto atatanuka pembeni. katika nafasi ya kiungo haina mabadiliko makubwa, mabadiliko huenda ni kwa upande wa majukumu ya wachezaji mmoja mmoja, lakini watacheza kama walivyocheza na Mbabane katika mechi ya ugenini.

Kama kocha wa zamani wa Simba, Mzambia Patrick Phiri alivyoshauri, Simba inatakiwa kuwa na utimamu, na nidhamu ya hali juu kwani, Nkana wako vizuri japo na kwa upande wao, wanaogopa kukutana na mnyama. Wachezaji wote wakicheza kitimu na si kusubiri Nkana wafanye makosa, inatakiwa wawalazimishe kufanya makosa.

Siri kubwa ya ushindi wa Simba leo, ni kumiliki mpira, na hata wakiupoteza inabidi waurudishe katika himaya mara moja. Nakumbuka kocha wa Man City , Pep Guardiola aliulizwa anataka wachezaji wake wafanye nini wanapokuwa hawana mpira naye akajibu hivi

 “ nataka wawe kama mbwa wanaoukimbiza mfupa na ni lazima waupate haraka iwezekanavyo”

Bila shaka viungo wa Simba leo inatakiwa wakawe kama mbwa wanaoukimbiza mfupa kipindi timu inapokosa umiliki wa mpira. Bila kusahau kushambulia kwa kasi wanapofika eneo la mpinzani yaani nusu ya uwanja. Mfumo huu wa kushambulia kwa kasi una mafanikio makubwa duniani ndio uliompa mafanikio makubwa Pep Gurdiola akiwa na Barcelona, Bayern na hata Man City.

Simba leo natarajia wataingia na mfumo wa 4-3-3 na Nkana wataanza na mfumo kipozeo 4-4-2. Yaani mfumo wa kuja kumzima 4-3-3. Mfumo wa Simba ni bora mbele ya 4-4-2 kwakuwa mfumo wa 4-4-2 unawafanya wachezaji wajitawanye uwanja mzima na huu ndio mfumo unaotumiwa na timu nyingi zinazoshambulia kupitia pembeni  lakini 4-3-3, viungo ndio muhimili wa timu, yaani hufanya timu imiliki mpira kwa muda mrefu na kutengeneza nafasi za kufunga.

Mabeki wa Simba wanatakiwa kuepuka makosa madogo madogo, na kadi zisizo za lazima hazina tija kwa timu kwani hushusha morari ya timu na upambanaji. Katika mchezo wa ugenini itapendeza kama Simba itapata matokeo. Kila la heri Simba.

Sambaza....