Sambaza....

Unakumbuka lile goli maridadi la kisigino la Mwamba wa Lusaka December 23 dhidi ya Nkana Red Devils pale kwa Mkapa ambalo lilipelekea Simba katika hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Africa baada ya muda mrefu kupita!?

Halafu kuna lile goli tena la Triple C palepale kwa Mkapa dhidi ya AS Vita lililoipa Simba ushindi wa mabao mawili kwa moja na kuipelekea Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka mingi kupita!

Clatous Chama (katikati) akishangilia.

Pia kuna lile goli la Lusi Miquissone dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa kwanza tu hatua makundi ya Ligi ya Mabingwa katika msimu uliopita na kupelekea Simba kumaliza vinara wa kundi mbele ya wababe kama As Vita na El-Merreck.

YouTube player


Yes ni Simba pekee ndio wameweza kuifanyaa hii kazi kwa ufasaha kabisa katika miaka ya hivi karibuni katika michuano mikubwa kabisa ya Afrika kwa ngazi ya vilabu. Ndani ya miaka mitano katika soka la Kimataifa Klabu ya Simba imecheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili na robo fainali ya kombe la Shirikisho mara moja.
Jonas mkude akimnyanyasa kiungo wa Al-Ahly.

Hii hii Simba ndio iliyotuletea miamba mbalimbali ya soka nchini kwetu, tumefanikiwa kupata burudani ya soka kutoka katika vilabu vikubwa Afrika kama Al-Ahly, Asec Memosa, AS Vita, El-Merreck, Nkana, Kaizer Chiefs, TP-Mazembe nasasa tunawasubiri Orlando Pirates “Amabakabaka” kutoka Afrika Kusini.

Simba hii ndio klabu ya kwanza kutoka Tanzania kupata ushindi ugenini nchini Congo, lakini pia kupata alama katika nchi za Nigeria na Sudan, na kuvitambia vilabu vya nchi za Kusini kama Swaziland, Botswana na Zambia.

John Bocco akiwa katika harakati za kumtoka mlinzi wa TP Mazembe.

Achana na hayo tujee huku kwenye teknolojia ambapo mchezo wa soka nao umejikuta ukikutana na hiyo kasi.

Simba inakwenda kuwa timu ya kwanza kutumia teknolojia ya VAR (Video Assistant Refferee) katika mchezo wa soka hapa nchini tena katika uwanja wa nyumbani.

Shirikisho la soka Barani Afrika yaani CAF ilitangaza kutumika kwa VAR katika michezo yake yote ya robo fainali kwa ngazi za vilabu kuanzia msimu huu ambapo Simba ni mshiriki pia katika michuank hiyo.



Simba inakwenda kucheza na Orlandio Pirates katika robo fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kwa Mkapa April 17 mwaka huu yaani Jumapili hii. Katika mchezo huo kutakua na matumizi ya VAR ili kutoa msaada kwa waamuzi wa mchezo huo.

Waamuzi watakaocheza mchezo huo wa ni mwamuzi wa kati Haythem Guirat kutoka Tunisia wasaidizi ni Khalil Hassani (Tunisia), Samuel Pwadutakam (Nigeria), Sadom Selmi (Tunisia), msaidizi wa video, Ahmed Elghandour (Misri) na msaidizi wa VAR Youssef Wahid Youssef (Misri).

Twenzetu kwa Mkapa tukaendee kuziishi ndoto zetu ambazo Simba wanazifanya kuwa kweli, twende kwa Mkapa tukaone tamu na chungu ya VAR yake kwa mara ya kwanza “live”, maana wanasema VAR haina rafiki wala adui wa kudumu.

Wachezaji wa Simba wakishangilia mbele ya mashabiki wao.

Kitu kizuri kwa mashabiki wa Simba na Tanzania kwa ujumla ni kuruhusiwa na CAF kuujaza uwanja wa Mkapa, yaani kwa Mkapa itakua ni “Full House”. Mashabiki 60,000 watakua uwanjani si tu kuitazama VAR kwa mara ya kwanza lakini pia kwenda kuisapoti Simba katika kutafuta ushindi mnono mbele ya Orlando Pirates.

Ni wazi sasa mashabiki wa Simba wamepata mtoko wa Pasaka kwenda kwa Mkapa si tu kutimiza ndoto ya kuitazama VAR kwa mara ya kwanza lakini pia kutimiza ndoto ya kwenda kufuzu nusu fainali katika michuano hii mikubwa Afrika.



Baada ya kushindwa kufuzu kwenda nusu fainali mara mbili katika Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa ni wazi ni wakati wa Simba kwenda kuandika historia mpya katika mchezo wa Jumapili kwa kupata ushindi mnono wa idadi kubwa ya mabao yatakayokua mtaji katika mchezo wa marudiano utakaopigwa April 24 nchini Afrika Kusini.

Twenzetu kwa Mkapa tukatimize ndoto zetu, twende kwa Mkapa tukaishi ndoto zetu zinazofanywa kuwa kweli na Wekundu wa Msimbazi Simba!

Sambaza....