Timu ya As Kigali kutoka Rwanda leo ilikuwa dimbani, uwanja wa taifa kuumana na Watoto wa Kinondoni KMC katika mchezo wa marudiano shirikisho Afrika na kuibuka na ushindi wa goli 2-1.
Haruna Niyonzima ni miongoni mwa waliokuwa katika msafara wa AS Kigali, licha ya kutocheza kutokana na kutopata leseni ya Caf ya kumruhusu kucheza lakini alikuwa bega kwa bega na timu yake mpya kuhakikisha inapata matokeo.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, Niyonzima amesema kuwa katika kitu ambacho anakipenda na bado atakikumbuka kwa muda wote wa maisha yake ni mapenzi ya dhati ya watanzania katika mchezo wa mpira miguu.
Haruna amesema kuwa ni dhahili bila kificho kuwa Watanzania wanaupenda sana mpira kuliko nchi zingine. Niyonzima ameendelea kwa kusema kuwa mapenzi hayo ni vigumu sana kuyakuta kwa nchi nyingine za kiafrika.
Aidha, Niyonzima hakuacha kuzitakia kila la heri
klabu zake mbili za zamani yaani Simba na Yanga kuelekea michezo yao ya
kimataifa. Yanga itakuwa uwanjani siku ya Jumamosi kukipiga na Township Rollers
ugenini huku Simba itaikaribisha UD Songo siku ya Jumapili uwanja wa taifa
ikiwa ni michezo ya marudiano klabu bingwa Afrika.