Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limemfuta kazi mkurugenzi wa Ufundi wa shirikisho hilo Amy Ninje kwa kile kinachoaminika kuwa ni sababu za kifamilia. Akitangaza uamuzi huo Rais wa TFF leo wakati wa uzinduzi wa jezi za timu ya Taifa Tanzania, amesema kuwa licha ya kuondoka kwake bado shirikisho litaendelea kumtumia katika mambo mbalimbali.
Kwa upande wa Ninje yeye atarudi nchini Uingereza kuungana na familia yake.
Swali kubwa muda huu ni nani ambaye atachukua nafasi hii muhimu yenye majukumu mazito kupeleka soka letu mbele? Inawezekana ikawa Oscar Mirambo, ambaye bechi lake la ufundi la Serengeti Boys ambalo lilikuwa likiongozwa na yeye kuvunjwa rasmi leo.
Lakini je Oscar anatosha katika viatu hivi?
Hebu tuangalie majukumu makuu ya Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho:
-Mipango ya maendeleo na programu husika za maendeleo ya soka
-Mafunzo ya makocha na Waamuzi
-Soka la Vijana
-Soka la Wanawake
-Mipango mkakati ya maendeleo ya mpira wa miguu
Kandanda imeongea na Tigana Lukinja, mwalimu wa mpira wa miguu na mchambuzi wa Radio na Televisheni “Mkurugenzi wa ufundi anapaswa kuwa Mchezaji wa siku za nyuma(former player. Itapendeza ikiwa ana taaluma ya kufundisha mpira wa miguu na kama kasoma Sports Management inakuwa safi zaidi , kifupi anapaswa kuwa na uweledi mpana wa Soka katika maeneo haya mawili”. Hivyo kwa nafasi hii Mirambo anaweza akatosha katika nafasi hii.
Uzoefu wa soka letu, na aina ya wachezaji wake na mazingira anaweza kuwa anayafahamu vizuri zaidi. Oscar Mirambo pia amewahi kukaimu nafasi hiyo kabla ya Ninje kuchukua majukumu hata.