Beki wa timu ya Soka ya Yanga Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amesema anaendelea kujifunza kutoka kwa wachezaji wenzake tangu alipojiunga na klabu hiyo miaka miwili iliyopita akitokea kisiwani Unguja.
Ninja amesema pamoja na kutazamwa kama mrithi wa aliyekua nahodha na beki klabuni hapo Nadir Haroub Canavaro, lakini anaamini Bado kuna mambo mengia mbayo anapaswa kuyafahamu hususani yanayohusu ushindani katika soka la Tanzania bara, na anaamini atafanikiwa.
“Bado sijaonesha vile alivyokuwa Cannavaro ila nimeahidi kuwa nitajitahidi niweze kufanya kama vile alivyokuwa kaka yangu Nadir Cannavaro,”.
“Nilichokiona kwenye kikosi cha Yanga ni ushindani wa namba, kinachonihamasisha zaidi ni kwamba toka nijiunge Nimeikuta Yanga ikiwa katika kipindi kigumu zaidi ila tunajitahidi wachezaji kupeana moyo tuweze kufikia malengo yetu,” amesema.
Katika hatua nyingine beki huyo amezungumzia mchezo wao dhidi ya Mbao FC ambao utachezwa Jumapili kwa kusema, wanaendelea kujiandaa na dhumuni lao kubwa ni kuhakikisha wanarejea katika furaha ya ushindi, baada ya kulazimisha suluhu ya bila kufungana dhidi ya Simba SC mwishoni mwa juma lililopita.
“Ninachokiona ni kuwa mchezo utakuwa mgumu, maana ukitizamana Mbao wamekuwa wakitufunga japokuwa hapa Dar hawajawahi kutufunga, halafu ukitazama waliweza kuwafunga Simba, nahisi wakikutana na sisi watazidi kutaka kupata matokeo ili wazidi kuonesha kuwa wamezifunga timu zote kubwa,” Ninja amesema.
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika katika Dimba la Taifa Jijini Dar es Salaam kuanzia saa moja jioni.