Sambaza....

MWAKA 2004 nikiwa U18 nilikuwa sehemu ya kikosi cha Jamaica FC ya Mkoani Morogoro. Katika moja ya siku mbaya katika maisha yangu ya soka ilikuwa wakati kocha Ally Jangalu aliponifanyia mabadiliko dakika tano kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza.

Ilikuwa ni katika mchezo wa kirafiki ndani ya uwanja wa Umoja, Mpwapwa dhidi ya iliyokuwa timu ya ligi kuu Tanzania Bara- Mji Mpwapwa FC.

Mwalimu Jangalu alinipanga nafasi ya beki wa kulia- sehemu ambayo licha ya kumudu kuicheza ila sikuwa nikiifurahia kupangwa. Nilipenda kucheza nafasi yoyote ya kati. Namba kumi, nane, sita ama beki yoyote ya kati, au upande wowote wa kushoto.

Mji Mpwapwa wakati huo walikuwa na winga mmoja hatari sana-namba 11 na ni huyo jamaa ´aliyenichongea´ . Ndani ya nusu saa nilikuwa ´hoi´. Niliwaomba wachezaji wenzangu wawili (Namba 3, na namba 6) tubadilishane nafasi lakini wote walinikatalia.

Nilitaka kubadili namba kwasababu mbili muhimu. Kwanza kumkimbia winga yule wa Mji Mpwapwa ambaye kasi yake nilishindwa kuimudu. Pili, nilikuwa nimechoshwa na kelele zilizoambatana na lugha kali zisizo na ´staha´ kutoka kwa Mwalimu Jangalu.

Kufikia dakika ya 40 kocha alinitoa na kumpa nafasi mchezaji mwingine. Nilichukia sana kwasababu licha ya usumbufu wa winga huyo hadi nafanyiwa mabadiliko matokeo yalikuwa 0-0.

Pamoja na udogo wangu nilijikuta nikimshambulia kwa maneno makali pia kocha wangu Jangalu (sasa ni kocha msaidizi wa Kagera Sugar FC, pia amewahi kufundisha Coastal Union)

Wakati nipo kwenye benchi nilimwambia Said Iddi (kiungo wa zamani wa Mtibwa Sugar FC na Reli FC), ” Sitaendelea kucheza timu hii tutakaporejea Morogoro”

Iddi alikuwa akimalizia soka lake na alikuwa mchezaji mwenye nidhamu ya hali ya juu mno, pia busara. Akaniuliza, “Utaenda kucheza wapi wakati tayari umesaini hapa?”

Kwa vile nilikuwa na hasira nikamwambia, ” Nitarudi kucheza Kingalu Kids- timu ya vijana wenzangu lakini si kucheza chini ya Jangalu.”

Baadae wakati tumerejea hotelini, usiku Said Iddi akanifuata na kuniambia kocha ananiita. Nikaenda kumsikiliza. ” Jiandae, kesho utaanza tena katika nafasi ya namba mbili dhidi ya Mpwapwa Kombaini na jua utakutana na mtu yuleyule kwasababu yupo pia katika timu ya Mpwapwa.” aliniambia, Jangalu mara baada ya kuitikia wito wake.

Baada ya kutoka kuzungumza na kocha, Said Iddi aliniambia twende ukumbini tukatazame Tv.

Tulipokuwa tumetulia akaniambia,
“Mdogo wangu kwanza futa mawazo ya kuondoka kwenye timu. Leo umecheza vibaya, hukuwa ukijiamini kama ulivyozoeleka, na hilo lilichangia kushindwa kwako kumdhibiti yule jamaa wa Mji. ”

” Unachotakiwa kufanya kesho ni kuondoa hofu tu. Yule ana kasi, nguvu na uzoefu zaidi yako hivyo unatakiwa kucheza karibu yake hasa timu yao inapokuwa na mpira. Usijali kufanyiwa mabadiliko mapema, mchezaji anaweza kutolewa hata ndani ya dakika tano kwa manufaa ya timu. Usighafilike kwa hili lililotokea Leo. Umepewa nafasi nyingine, kasahihishe makosa.”

Nilimsikiliza kwa makini yule kakayangu wa mpira. Kesho yake niliweza kucheza vizuri mno na nilifanikiwa kudhibiti harakati zote za yule winga wa Mji Mpwapwa na baada ya mechi alinifuata na kunipongeza.

CLAUS KINDOKI

Kipa huyo raia wa Congo DR alionekana kulia kwa uchungu wakati akiwa katika benchi la wachezaji wa akiba wa Yanga baada ya Alhamis iliyopita kuruhusu goli linalotajwa ni ´la uzembe wake´ wakati wa mchezo wa Mwadui FC 1-2 Yanga.

Kindoki alishindwa kudhibiti shuti lililopigwa na Charles Ilamfya ambalo aliutema mpira huo uliomaliziwa na Salim Aiyee na kuisawazishia Mwadui.

Lilikuwa ni goli la nne kufungwa kipa huyo katika michezo yake minne ya ligi kuu – ikiwemo ´Hat Trick´ aliyofungwa na Mrundi, Kitenge katika mchezo wake wa kwanza tu akiichezea Yanga.

Ni kweli mashabiki hawapendi kuona wachezaji wao wakifanya makosa mara kwa mara- hasa makosa hayo yanaposababisha madhara kwa timu yao.

Mashabiki wa Yanga walishinikiza kutolewa kwa Kindoki mara baada ya makosa yake kuipa Mwadui FC goli la kusawazisha. Kocha Zahera Mwinyi alimtoa kipa huyo na nafasi yake kuchukuliwa na yosso, Ramadhani Kabwili.

Kindoki tayari amepoteza imani kwa mashabiki, na kama benchi la ufundi nalo litapoteza imani kwa nyanda huyo watakuwa ni sawa na kummaliza kabisa. Wamsaidie na si kumuacha na machozi yake.

Kindoki mazoezini

Wamsaidie kwa kukaa nae na kumwambia anaweza kunyanyuka baada ya kuteleza. Kwa namna alivyokuwa akilia ni wazi asiposaidiwa kisaikolojia atatamani kuondoka ndani ya timu kwa sababu anajitazama kama sababu ya kuanguka kwa timu.

Inawezeka asiwe kipa wa kiwango cha juu, lakini apaswi kuachwa apotee zaidi. Wamsaidie sasa. Kwa kumwambia anaweza kusahihisha makosa yake na kuwa bora.

Sambaza....