Hatimae wababe wawili wakucheza fainali ya Azamsports Federation Cup wamepatikana mwishoni mwa wiki hii baada ya Coastal Union kufanikiwa kuiondosha Azam Fc katika nusu fainali ya pili.
Coastal Union wanaungana na Yanga kucheza fainali ya kombe hilo baada ya kuiondosha Azam Fc kwa mikwaju ya matuta baada ya dakika 120 kuisha kwa suluhu.
Katika mchezo huo wa nusu fainali ya pili uliyopigwa Sheikh Amri Abeid Arusha Coastal Union walikua na kila sababu ya kuvuka na kwenda fainali kutokana na kiwango kizuri walichokionyesha ndani ya dakika 120 za mchezo.
Vijana wa Juma Mgunda walipaswa wajilaumu wenyewe kama wangepoteza mchezo huo kwani walitengeneza nafasi kibao za wazi lakini washambuliaji wake wakashindwa kuzitumia.
Katika mikwaju ya matuta ni Lusajo Mwaikenda na Charles Zulu ndio walikosa mikwaju yao ya penati na kuepelea Coastal kwenda fainali.
Coastal Union sasa ataungana na Yanga kucheza mchezo wa fainali utakaopigwa July 2 katika dimba hilohilo la Sheikh Amri Abeid. Yanga alishatangulia fainali baada ya kumfunga Simba bao moja bila CCM Kirumba Mwanza.