NDIO kwanza ametimiza miaka 41 siku ya Alhamis hii, mzaliwa wa Bunjumbura, Burundi, Masoud Djuma bila shaka ameshajitambulisha kwa wapenzi wa soka nchini kwa stahili yake ya ‘kushambulia na kuzua kwa kutumia mabeki’.
Muda mwingi wa mchezo Djuma amekuwa akisimama karibu na uwanja huku akitoa maelekezo kwa wachezaji japo stahili hiyo wakati mwingine huwachanganya zaidi wachezaji uwanjani na kuona kama wakipigiwa kelele. Ni kocha muhamasishaji na ambaye timu yake inapokuwa katika ubora utaliona tabasamu lisilo la kinafki.
Kwa miaka 18 sasa nimekuwa mfuatiliaji wa vikosi cha Simba SC. Bado hakuna kocha ambaye aliweza kuifanya Simba kucheza vizuri zaidi huku ikipata matokeo katika karne hii kama Mkenya, James Siang’a ( mwenyezi Mungu amrehemu) na kikosi chake cha mwaka 2003 ambacho kilifika hatua ya makundi Caf Champions League kwa mara ya kwanza na ya mwisho kilivutia mno kutazama.
4-4-2 ulikuwa mfumo ambao Siang’a – golikipa wa zamani wa Kenya aliutumia kuweka rekodi zake ambazo zinaendelea kuishi hadi sasa. Alishinda mataji matatu ya ligi kuu ( 2001, 2003 na 2004) taji moja la Cecafa Kagame Cup ( 2001) ligi kuu ya Tanzania-Ligi ya Muungano ( 2002), mataji matatu ya Tusker Cup ( 2001, 2002, 2004), taji moja la Hedex Cup na mara zote Simba ilicheza soka la ‘tamaduni yao’ –mpira wa chini, kasi na ufundi, huku timu ikicheza katika uwiano sawa kiulinzi na mashambulizi.
Pengine Mkenya huyo aliyetangulia mbele ya haki asingekutana na ‘mafionso’ wa soka la Tanzania angeweza kufika walau fainali ya kikombe kimojawapo barani Afrika. Nilipenda vikosi vyake ambavyo viliendeleza utamuduni wa kiuchezaji wa klabu.
Patrick Phiri raia wa Zambia ambaye alichukua nafasi ya Siang’a kwa mara ya kwanza mwaka 2004, aliendeleza uchezaji wa kuvutia wa klabu lakini yeye alitumia mifumo miwili; 4-4-2 na mara nyingi 4-3-3 lakini licha ya kufanikiwa kushinda ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara pasipo kupoteza mchezo msimu wa 2009/10, kikosi cha Mserbia Milovan Curkovic kilichoshinda ligi kuu na kukaribia kufuzu nane bora ya Caf Confederations Cup msimu wa 2011/12 kilicheza vizuri mno katika mfumo wa 4-3-3 kuliko kile cha Phiri ambacho kiliondolewa na TP Mazembe katika ligi ya mabingwa Machi 2011.
Makocha pekee ambao ‘walioboa’ na mchezo wao ndani ya Simba ni Msauz, Trott Moloto ( 2005) na Mcameroon, Joseph Omog ( Agosti 2016-Januari 2018). Kuna makocha ambao waliangushwa kwa makusudi na baadhi ya watu wa Simba yenyewe na bahati mbaya kwao walifanya hivyo kwa makocha ambao waliweza kuipa mchezo wa kuvutia na mataji ya ndani huku vikosi vyao vikipambana vizuri Caf- Siang’a na Phiri ni mfano sahihi kwa karne hii.
Milovan licha ya kuwa kocha mzuri kimbinu na ufundishaji lakini yeye hakuwa mtu mwenye kujali nidhamu yake na ile ya wachezaji, aliweza kufundisha-ndio, lakini alikuwa mtu anayependa kujirusha mno tena bila kificho. Hata kama kuna wakati alilalamika kuingiliwa katika majukumu yake lakini huyu ni kati ya wale waliojiangusha wenyewe japo aliendena vizuri na tamaduni ya kiuchezaji wa klabu.
DJUMA…..
Ni kijana mwenye kutaka kazi yake ionekane bora siku zote. Wakati anakuja Simba mwishoni mwa mwaka uliopita ilisemwa kuwa atakuwa msaidizi wa Omog ambaye alikuwa peke yake baada ya Mganda, Jackson Mayanja kujiuzulu mwanzoni tu mwa msimu. Wengi walitia shaka, na iliaminika Djuma amekubali kuondoka Rayon Sports aliyokuwa ameipa ubingwa wa Rwanda kama kocha mkuu ili kuchukua kibarua cha Omog.
–Bandiko la Msemaji wa klabu ya Simba katika ukursa wa Instagram
Uongozi ulificha na baadae ukaona aibu kumtimua Omog kwa kuwa kuna watu walihoji unaweza vipi kumuondoa kocha ambaye amepoteza ligi kwa kuzidiwa magoli ya kufunga na kufungwa, huku akiwa juu ya msimamo katika msimu mpya. Mara zote nilisisitiza Omog anapaswa kufukuzwa kwa sababu hakuwahi kuifanya Simba ipate matokeop katika utaratibu wa klabu-kiuchezaji.
Kitendo cha kuondolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penalty na Green Warrios ya ligi daraja la pili Januari iliyopita siku ya kwanza wanatia mguu kutetea ubingwa wa FA, Djuma alionekana kutamani zaidi nafasi ya ukocha mkuu na kwa aina ya mbinu na uchezaji wa vikosi vyake ndani ya Simba Mrundi huyu hapaswi kuwa kocha msaidizi na pengine hata yeye anaamini hivyo.
PESA….
Palipo na pesa siku zote ndipo pajaapo watu. Djuma alikubali ‘kivuli cha ukocha usaidizi Simba’ kwasababu pesa ilitumika kumlaghai. Na mwanahisa mkuu wa klabu kwa mawazo yake anaamini Simba ili kuwa klabu bora na yenye ushindani katika michuano ya Caf ni lazima iwe na kocha mwenye wasifu m,kubwa duniani. Hii ndio sababu badala ya kumpa kazi Djuma mara baada ya kuondoka kwa Omog wakampatia Mfaransa, Pierre Lechantre.
Kiuchezaji vikosi vya Lechantre ndani ya Simba havikucheza vizuri zaidi ya vile ambavyo vilisimamiwa na Djuma kwa nyakati tofauto Omog alipokosekana. Rejea Ndanda FC 0-2 Simba, Kagera Sugar FC 0-2 Simba msimu uliopita, na kuthibitisha Lechantre hakuwa mkali zaidi ya Djuma rejea Simba vs Azam FC, na Simba vs Yanga ( game za marejeo msimu uliopita)
3-5-2 ni mfumo ambao niliukosoa sana wakati Djuma alipoanza kuutumia kwa sababu niliamini mfumo huu unahitaji kikosi hasa kilichosainiwa na mwalimu mwenyewe, lakini Mrundi huyu aliweza kutengeneza kiungo kigumu akiwatumia mara kwa mara, Waghana, Niclos Gyan, James Kotei, Erasto Nyoni, Jonas Mkude na Shiza Kichuya.
Aliposajiliwa Mghana mwingine Asante Kwassi na kurejea kwa u-fit wa Shomari Kapombe Simba ilicheza vizuri mno katika mfumo huo licha ya kwanza si utamaduni wa klabu. Niliona wakati Big Phill akiipa Brazil ubingwa wa dunia wakicheza vizuri katika 3-5-2, niliona pia kikosi bora zaidi cha Milan AC katika karne mpya chini ya Carlo Ancelotti kikitwaa taji la mabingwa ulaya huku kikicheza soka la kiwango cha juu katika 3-5-2.
Licha ya kumpinga Djuma wakati anaingia na mfumo huo Simba lakini kama angeaminiwa na kupewa nafasi ya kufanya usajili wake pengine angeweza kutengeneza historia yake lakini pesa wakati mwingine inashinda tamaa.
Habari kwamba kocha huyo amekuwa ‘kirusi’ ndani ya Simba ambacho kinazalisha mipasuko ya ndani kati ya wachezaji na kocha mkuu Mbelgiji, Patrick Aussems zimeanza kuvuja mara baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo , Mfaransa Lechantre kufanya mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini na kusema, Djuma anatamaa ya ukocha mkuu na alikuwa akishriki kumuhujumu wakati walipokuwa wakifanya kazi pamoja kati ya Januari hadi Juni mwaka huu.
Hili la tama ya ukocha mkuu wala halina kificho kwa Djuma, nakumbuka wakati Lechantre na Omog walipoondolewa alisisitiza anahitaji kazi hiyo na amekuwa akijisifu kuwa anaweza kuipaisha mno Simba. Kwa mtazamo wa kawaida Simba wanajua ni kwanini walimleta Djuma- hata kama wanaficha lakini beki huyo wa zamani wa Burundi walimtoa Rayon ili awe kocha mkuu lakini sasa wanaamini wanahitaji ‘wasifu mkubwa zaidi wa kocha wao’ na si kocha ambaye hajawahi kucheza michuano mikubwa ya Afrika.
Huu ndio wakati ambao uongozi wa Simba haupaswi kufichaficha mambo yanayoweza kuwaathiri huko mbeleni, wamuondoe tu Djuma japo wataonekana ‘wasariti’ kwa kocha huyo. Kuendelea kuwa naye ni makosa kwa sababu hawakumleta kuwa msaidizi bali kocha mkuu. Anaona yeye ni bora kuliko ‘wazungu wanaopapatikiwa’ na kulipwa mishahara mikubwa huku kiwango cha timu kikiwa chini uwanjani.
Kama pesa ndiyo ilimleta Patrick, ikazalisha usariti ni wakati sasa wa Simba kuitumia pesa hiyo kumuondoa Djuma kabla ya mambo kuharibika zaidi. Mzungu anaonekana naye anataka kufanya kazi ya timu yake ya ufundi hivyo ufanyike uamuzi sasa. Djuma aondolewe kwa maslai ya pande zote nne- Klabu, Patrick, Djuma na wachezaji hata kama kuna siri nyingi za usariti zitaanza kuvunja kutoka kwa Mrundi huyo kama alivyofanya Lechantre.