Waswahili hutumia neno “Gundu” kwa kuashiria bahati mbaya, kukosa bahati ama mkosi, ndicho unachoweza kusema kwa timu zote mbili Simba na Yanga kuelekea mchezo wao wa nusu fainali wa Azam Sports Federation Cup.
Ndio ni Gundu kwa maana ya vikosi vyote viwili kutarajiwa kukosa wachezaji wake muhimu katika mchezo wa nusu fainali kutokana na majeruhi waliyoyapata.
Balama Mapinduzi, Juma Abdul, Papy Tshishimbi ni wazi wataukosa mchezo huo huku Haruna Niyonzima akiwa 50/50 kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata katika mchezo dhidi ya Biashara United.
Kwa upande wa Simba ni mlinzi wao wa kulia Shomary Kapombe alieumia katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Azam fc pamoja na Rashid Juma wataukosa mchezo huo dhidi ya Yanga.
Ni Yanga ndio inaonekana kuathirika zaidi na majeruhi ya wachezaji wake haswa kutokana na kuwa na majeruhi wengi katika eneo la kiungo. Papy, Balama na Haruna wote wanacheza eneo la kiungo hivyo kuicha Yanga na machaguzi machache kuelekea mchezo huo. Ni Makame, Feisal, Ngassa na ujio wa Mo Banka alietoka majeruhi pia ndio wachezaji pekee wa eneo hilo walio baki kwa mchezo huo mpaka sasa.
Katika michezo miwili ya Ligi ya msimu huu dhidi ya Simba Haruna, Mapinduzi na Tshishimbi walicheza eneo la kiungo na kuepeleka Yanga kupata alama nne katika michezo yote miwili. Wachezaji hao walikua ndio eneo muhimu na la mkakati katika michezo yote miwili. Hivyo Yanga watapata pigo kubwa kuelekea mchezo huo kwa kuwakosa viungo wao muhimu.
Kwa upande wa Simba sasa hakuna namba Haruna Shamte “Terminator” atakwenda kuziba pengo la Shomary Kapombe kuelekea nusu fainali hiyo huku pia Mzamiru Yassin au Erasto Nyoni wanaweza kutumika katika upande wa kulia. Kwa Rashid Juma yeye ni kama hajaacha pengo lolote kutokana na utitiri wa wachezaji wanaocheza eneo la kiungo wa pembeni kwa Simba.