Sambaza....

Jana nilikuwa napitia maoni ya mashabiki wa Yanga, ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wanaonekana wana furaha sana. Furaha yao imejengwa kwa wao mpaka sasa hivi kutofungwa katika mechi 9 walizocheza.

Ni mwanzo mzuri sana wa ligi, mwanzo ambao unatia matumaini sana, na ni mwanzo ambao Mwinyi Zahera na kikosi chake kinastahili sana pongezi. Najua mechi nyingi wamecheza katika uwanja wa Taifa. Watu wanasubiri kuwaona nje ya uwanja wa Taifa, lakini kwa hatua hii ambao wamefika wanastahili sana pongezi.

Makambo

Kuutumia uwanja wa nyumbani ni Sanaa kubwa inayohitaji maarifa, wamebakiza sanaa ya kutumia uwanja wa ugenini, sanaa ambayo inahitaji maarifa mengi, maarifa ambayo naamini washajiandaa!.

Maandalizi ni kitu cha muhimu sana kwenye ligi hii yenye mechi 38. Mechi ambazo ni nyingi sana, mechi ambazo zinahitaji upana wa kikosi na siyo rundo la wachezaji.

Tafasri halisi ya neno kikosi kipàna siyo kuwa na wachezaji wengi kwenye kikosi, bali kuwa na wachezaji wengi ambao wanalingana au kupishana kidogo sana uwezo. Kiasi kwamba kocha anakuwa na mbadala sahihi.

Mechi mbili zilizopita za Yanga (Mechi dhidi ya KMC na mechi dhidi ya Lipuli iliyochezwa Jana) ilionesha Yanga wanakikosi finyu, kikosi chenye rundo la wachezaji wenye kiwango cha kawaida. Kwa kifupi Yanga ina rundo la wachezaji wa kawaida sana!.

Kwanini nasema hivo ?. Mechi hizo mbili zilizopita ambazo nimezitaja, tumeishuhudia Yanga ambayo inacheza bila Ibrahim Ajib, mchezaji ambaye kabla hajapata majeraha alikuwa amehusika katika magoli 11 kati ya magoli 14 ya Yanga.Kwa kifupi mpaka sasa amehusika katika magoli 11 kati ya magoli 16 ya Yanga.

Hajahusika moja kwa moja kwenye magoli matano tu!, hii inatosha kuonesha huyu ndiye mhimili mkubwa katika ubunifu wa upatikanaji wa magoli katika timu ya Yanga.

Alipata majeraha , akakosekana katika hiyo michezo, michezo ambayo Yanga ilishinda kwa ushindi wa goli 1-0 katika kila mchezo. Ushindi mwembamba sana!, pamoja na kwamba walipata ushindi mwembamba pia utengenezaji wa nafasi ulikuwa ni finyu sana.

Mechi zote mbili Yanga imehangaika kutengeneza nafasi katika hizo mechi mbili alizokosekana Ajib , hasa hasa nafasi ambazo zinaonekana ni za wazi.

Jiulize mbadala wa Ajib ni nani ?, na vipi anakiwango kinachokaribiana na Ajib?. Ukijiuliza maswali hayo ndipo utakapoona Yanga ina kikosi finyu sana. Ni sawa na pale utakapoamua kupoteza muda wako na kujiuliza kama siku Faisal Salum Fei “Toto” akiumia. Nani atakuwa mbadala wake ?, vipi mpishano wa kiwango ukoje ?.

Kuna wakati Yanga iliwahi kuwa na Amis Tambwe yule wa kipindi kile, kipindi ambacho alikuwa hatari sana, wakawa na Donald Ngoma. Yule mshambuliaji aliyekuwa anaogofya, pembeni yake alikuwepo Simon Msuva yule aliyekuwa anatoka pembeni na kufunga huku Obrey Chirwa akikamlisha listi ya upana wa kikosi.

Hadithi hii ni tofauti sana kwa sasa katika kikosi cha Yanga, ila hadithi hii inafanana sana na hadithi ya upande wa pili wa mahasimu wao Simba.

Ambao wana Emmanuel Okwi aliyewa moto, John Bocco anayetisha, Meddie Kagere ambaye ni hatari huku Adam Salamba aliyekatika kiwango bora kabisa. Wote hawa mpaka sasa wamefunga jumla ya magoli kumi na nane tu. Magoli 18 yametoka kwa hawa wanne tu

Wakati Makambo, Ibrahim Ajib, Mrisho Ngassa na Deus Kaseke wamefunga jumla ya goli kumi tu mpaka sasa. Huu ndiyo utofauti unaowatofautisha hawa. Hata eneo la kiungo Simba ina utajiri sana. Tumeona Mkude na Kotei wamekosekana katika mechi mbili lakini Said Ndemla aliingia na kucheza katika kiwango bora.

Wachezaji wa Yanga wakipongezana katika moja ya mechi

Turudi hapa kwa Makambo!, huyu ndiye mshambuliaji ambaye anategemewa kwa sasa timu ya Yanga. Wamefunga magoli manne. Lakini mpaka sasa hajaonesha ukomavu wa yeye kuibeba timu yake, kwanini nasema hivo ?. Amekuwa mchezaji ambaye anakosa nafasi nyingi sana. Afu siyo aina ya washambuliaji ambao wanaweza kuibeba timu.

Kuna wakati timu huwa inabanwa sana, ndiyo wakati ambao huitajika Musa wa kuibeba timu mpaka Kanani. Hiki kitu Makambo hakiwezi. Hawezi kabisa kuibeba timu na kibaya zaidi hata wachezaji wanaomzunguka wana hawana uwezo mkubwa sana.

Mrisho Ngassa siyule wa miaka ile, Deus Kaseke hana maamuzi mazuri ya mwisho. Anaweza kukufurahisha kwa kufanya vizuri mwanzoni lakini anapoenda kumalizia kazi ya mwanzo maamuzi yake ya mwisho yanaweza kukufanya utoe tusi kubwa mdomoni mwako.

Yupi mbadala wa Makambo ?, Amis Tambwe? Mtu ambaye hupata majeraha ya Mara kwa Mara hata kiwango chake kinaonekana kimepungua sana. Kwa kifupi kiwango cha Makambo na ufinyu wa kikosi cha Yanga hakitoshi kuwapa Yanga Ubingwa. Wanachotakiwa ni wao kulitumia vizuri dirisha dogo la usajili!.

Sambaza....