Unaona sasa, baada ya jana Taifa Stars kuichapa Niger 1-0, na Algeria kuifuga Uganda 2-1, kinachofuata ni hesabu kali na roho mbaya ili Tanzania ikacheze Afcon kwa mara ya tatu.
Matokeo ya jana yameifanya Taifa Stars kufikisha alama saba nafasi ya pili nyuma ya Algeria iliyofuzu tayari na alama 15, Uganda ikiwa ya tatu na alama nne na Niger ikiburuza mkia na pointi mbili huku kila timu ikiwa imebakiza mechi moja.
Taifa Stars itamaliza na Algeria ugenini huku Uganda pia watakua ugenini ili kwenda kumalizana na Niger pia.
Katika mechi hizo, Stars inahitaji sare tu dhidi ya Algeria ugenini kwa maana ya alama moja ili iweze kufuzu na nje ya hapo ni roho mbaya tu itakayohitajika.
Naam! Roho mbaya hiyo ni pale ambapo Stars itashindwa kupata walau sare mbele ya Algeria basi Watanzania itabidi tuiombee dua mbaya Uganda nayo itoe sare au kufungwa na Niger. Inawezekana japo ni ngumu kutokea.
Hivyo ndivyo mpira ulivyo, tukikosa alama moja kwa Algeria kitakachofuata ni kuwawekea dua mbaya wenzetu majirani Uganda.
Mwisho tutasema Am Sorry and Thank You Uganda. Ni ngumu lakini inawezekana. Let’s go Taifa Stars.
Kumbuka Stars inatafuta kufuzu Afcon kwa mara ya tatu katika historia ya nchi, michuano hiyo imepanga kufanyika mwakani mwaka 2024 nchini Ivory Coast.