Sambaza....

Mshambuliaji wa wanarambaramba Azam FC Mzimbabwe Donald Ngoma anatarajiwa kurejea dimbani hivi karibuni licha ya taarifa ya klabu hiyo kuthibitisha kuwa bado mchezaji huyo hajaanza mazoezi na wenzake.

Kwa mujibu wa afisa habari wa Azam FC Jaffary Idd Maganga ni kwamba mchezaji huyo ambaye amejiunga mwezi Juni akitokea Yanga, bado anahitaji uangalizi wa madaktari lakini wanapata matumaini ya kuwa huenda akarejea uwanjani kwenye mechi ya raundi ya nne dhidi ya Mwadui FC.

Maganga amesema mbali na Ngoma pia hata beki Yakubu Mohamed hali yake inatia matumaini ya kurejea Uwanjani na kinachosubiriwa kwa sasa ni ‘Go Ahead’ kutoka kwa madaktari ili kuanza kuwatumia.

“Hawa walikuwa kwenye matibabu, na sasa hivi wanaendelea vizuri sana, tunachosubiri ni ruhusa tu ya daktari ya ni lini watajiunga na wenzao kwenye mazoezi,” Maganga amebainisha.

Akizungumzia umuhimu wao katika kikosi, Maganga amesema kurejea kwao kunawapa matumaini ya kuwa na kikosi kipana zaidi lakini pia morali kwa wachezaji inaweza kuongeza kwani wachezaji hao ni wazoefu na wana umuhimu mkubwa kwenye timu katika kupambani nafasi za juu katika ligi.

Mbali na hilo Maganga amethibitisha kuwa kutakuwepo kwa mchezo wa kirafiki baina yao na timu ya ligi daraja la kwanza kutoka Arusha, timu ya Arusha United mchezo utakaofanyika Jumanne kwenye uwanja wa Azam Complex.

Sambaza....