Haruna Moshi ” Boban” ni jina ambalo lilipata umaarufu sana, na ni jina ambalo lilikuwa linahusudiwa sana kuwepo kwenye midomo ya mashabiki wengi.
Na ndilo jina ambalo lilikuwa lina nguvu sana katika kikosi cha Simba. Vitu vyote hivi ni kwa sababu ya “ufundi” wa Haruna Moshi “Boban”.
Kwa kifupi huyu alikuwa ” fundi” wa mpira na bado anaendelea kuonesha “ufundi” wake akiwa na timu ya African Lyon.
Ndilo jina ambalo liliacha maswali kwanini halikuweza kucheza soka katika ligi za ulaya kwa kipindi kirefu kwa sababu Haruna Moshi “Boban” alikuwa amekamilika kwa kiasi kikubwa.
Ukamilifu ambao uliwafanya mashabiki wengi wa mpira kumfananisha na Zvonimir Boban kiungo na kapteni wa zamani wa Croatia ambaye kwa sasa ni katibu msaidizi wa FIFA.
Mshindi wa klabu bingwa Ulaya na mshindi wa medali ya mshindi wa tatu wa kombe la dunia.
Haruna Moshi alifanana vingi sana na kiungo huyu wa Croatia kuanzia nafasi ambayo alikuwa anacheza mpaka aina ya uchezaji.
Ufundi kwenye miguu ya Haruna Moshi “Boban” ilitupa imani kuwa atafika mbali, lakini akili yake ilituangusha.
Hakuwa na watu sahihi ambao walikuwa wanamzunguka. Watu ambao wangemwelekeza njia sahihi ya kupita.
Na kibaya zaidi hakuwa na msimamizi mzuri wa kipaji chake (meneja sahihi) ambaye angemkumbusha kuwa hakutakiwa kumaliza maisha yake ya kucheza mpira akiwa masikini.
Meneja ambaye angemkumbusha muda mzuri wa kupiga mazoezi binafsi, muda wa kupumzikia, chakula kizuri kwa kula na chakula au kinywaji ambacho siyo kizuri kwa kunywa.
Kwa kifupi hakuwa na watu bora ambao wangeibeba miguu yake na kuipeleka ulaya. Ndiyo maana Haruna Moshi “Boban” hakuitendea haki miguu yake kuiweka Tanzania kwa muda mrefu.
Hata alipojaribu kwenda kubahatisha bahati yake nje, aliikumbuka Tanzania hivo alirudi bila sababu za msingi.
Kwa kifupi nidhamu dhaifu ilimfanya Haruna Moshi “Boban” Leo hii achezee Africa Lyon akiwa hana mafanikio makubwa .
Umri umeenda, nguvu kwenye miguu imepungua kwa kiasi kikubwa, hawezi tena kushindana kwa kiasi kikubwa kama zamani.
Hawezi tena kuonesha ufundi wake wa hali ya juu kama zamani ingawa hajaisha kivile.
Bado ana kitu cha kuwafundisha kina Faisal Fei “Toto”. Inawezekana hawakubahatika kumuona kipindi ambacho yupo katika kiwango chake kikubwa.
Inawezekana walikutana na habari zake tu nyingi za kumsifia kiwango chake lakini mboni za macho yao hazikubahatika kumuona Haruna Moshi ” Boban”.
Naamini huu ndiyo wakati mzuri kwao wao kukaa chini na daftari pamoja na kalamu ili kunakiri kidogo ambacho kimebaki kwa Haruna Moshi “Boban”.
Uwezo mkubwa wa kuchezesha timu kwa akili kubwa. Uwezo wa kupiga pasi ambazo zinaleta madhara kwenye timu na ubunifu mkubwa wa kitengeneza nafasi za kufunga.
Kwa kifupi ni kwamva Haruna Moshi ” Boban” ni somo halisi la namna ambavyo kiungo mshambuliaji anatakiwa kuwa.
Pamoja na kwamba Haruna Moshi “Boban” anasomo zuri ndani ya uwanja mpaka muda huu lakini tusisahau kusoma ukurasa wa kitabu chake kinachoonesha kwanini alishindwa kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na kipaji chake?.
Kwanini hakufanikiwa kucheza nje licha ya kuwa na kipaji kikubwa katika miguu yake?
Hapana shaka neno “nidhamu” litabeba vitu vyote. Nidhamu ya kuheshimu kipaji chako. Mtu wa kwanza wa kukisimamia kipaji ni mchezaji husika.
Mchezaji anatakiwa ahakikishe kipaji chake kinapanda kwa kufanya mazoezi kwa bidii, kuonesha kiwango kikubwa ndani ya uwanja. Kuwa na muda mzuri wa kupumzikia, kutotumia vilevi na starehe hatarishi ya kipaji.
Kujitambua ni kitu cha msingi, wewe ni nani ? Kwanini Mungu amekuleta duniani? Unafanya nini ili kufikia kusudio la Mungu kukuleta duniani?
Kipi unakifanya ili ufike mbali na kuweka alama ambazo zinatazamika?, marafiki wako wanaokuzunguka wanakusaidia kupambana kwenda mbele au wanakurudisha nyuma?
Una timu sahihi ya kukusimamia kipaji chako ili ufike mbali? Haya ni baadhi ya maswali ambayo mchezaji mwenye njaa anatakiwa kujiuliza wakati anapambana kuzifikia ndoto zake.