Sambaza....

BAADA ya ushindi wa 16 katika michezo 18 ya mzunguko wa kwanza, pointi 50 mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania bara, Yanga SC wamesema wataifunga pia Azam FC katika mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza ili kutanua pengo lao la pointi.

Yanga iliifunga Mbeya City FC magoli 2-1 Jumamosi iliyopita na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama kumi dhidi ya wanaoshika nafasi ya pili Azam FC ambao walikumbana na kipigo cha kwanza msimu huu kutoka kwa Mtibwa Sugar FC siku ya Jumamosi.

” Hatujamaliza kazi ” anaanza kusema Mrisho Ngassa nilipofanya nae mahojiano mafupi jana Jumapili. ” Tulihitaji pointi zote tatu dhidi ya Mbeya City na tunamshukuru Mungu tumefanikiwa. Sasa tuna tazama washindani wetu wajao na lengo letu ni lilelile kushinda.”

Ngassa alicheza kwa kasi robo saa ya kwanza ya mchezo dhidi ya City, kocha Zahera Mwinyi aliwapanga ‘ maveterani’ wake Ngassa, Amis Tambwe na Haruna Moshi ‘Boban’ katika kikosi kilichoanza na wakafanikiwa kufunga magoli yote mawili katika kipindi cha kwanza.

” Ilikuwa ni jambo la kupenda kucheza kwa mara nyingine na Boban baada ya miaka mitano. Tulicheza pamoja tukiwa Simba msimu wa 2012/13 na nimefurahi kucheza nae timu moja kwa mara nyingine.”

Sambaza....