Sambaza....

Huku klabu ya soka ya Sevilla ikiwasili leo tayari kabisa kuikabili klabu ya soka ya Simba katika dimba la uwanja wa Taifa “Kwa Mkapa” siku ya Alhamis tayari kocha wa Simba ameanza kuwapigia hesabu Wahispania hao.

Katika moja ya mahesabu yake ni pamoja na kuwapumzisha wachezaji huku wakicheza kwa zamu ili kulinda utimamu wa miili yao kutokana na ratiba ngumu ya viporo wanayokabiliana nayo.

Lakini pia ili kunogesha utamu wa mchezo wa Kirafiki wa Kimataifa kati ya Simba sc na Sevilla pia mwalimu ameonekana kuwaandaa baadhi ya wachezaji kwaajili ya mchezo huo.

Kiungo Ever Banega akipiga penati katika moja mchezo wa Laliga.

Moja ya wachezaji wanaoonekana kuandaliwa kwa mchezo huo ni pamoja na kiungo fundi Said Khamis Ndemla “Daktari”. Ndemla katika michezo mitatu ya hivi karibuni amekua akitumika kama mchezaji wa akiba au kutokuwepo kabisa katika benchi la akiba.

Baadhi ya michezo aliyokosa Ndemla ni dhidi ya Ndanda fc na Singida Utd ambapo hakuepo kabisa hata katika benchi, lakini alikua mchezaji wa akiba katika michezo dhidi ya Azam fc na Mtibwa Sugar.

Ndemla amekua akitumika kama kiungo wa chini kwa sasa na mwalimu Patrick Aussems hivyo basi katika mchezo dhidi ya Sevilla huenda akawa katika kikosi cha kwanza na atakutana na nahodha wa Sevilla Ever Banega ambae hucheza eneo la nyuma ya mshambuliaji “Behind the striker” ama kiungo mshambuliaji.

Tutegemee kumuona Ndemla akikutana na mafundi wenzie kutoka Hispania katika eneo la kiungo siku ya Alhamis katika dimba la Mkapa.

Sambaza....