Kocha mkuu wa timu ya soka ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) Mrundi Etienne Ndayiragije amesema amependekeza kwa Uongozi kumuongezea wachezaji wanne katika dirisha hili dogo la Usajili ambalo limefunguliwa leo.
Ndayiragije amesema anataka kuwa na wachezaji wawili wawili katika kile nafasi na ndiyo maana amepeleka mapendekezo hayo Ili kuweza kujenga kikosi imara kitachopambana kwenye Ligi na mashindano mengine kama kombe la Shirikisho.
“Hili dirisha dogo tumependekeza kwa uongozi tuweze kuongeza nguvu kwenye eneo la Foward aina ya namba Tisa, pia na beki wa kushoto kwa sababu nina mmoja tu nahitaji kuongezea mwingine na nilihitaji namba sita kwa sababu aliyekuwepo ameondoka na nimebaki na mmoja, na beki wa kati pia kwasababu Yusuph Ndikumana amepata sana majeraha hivyo nahitaji kupata mwingine ili wasaidiane,” Ndayiragije amesema.
Ameongeza kuwa wachezaji wote aliowapendekeza hawatoki nje ya Tanzania na amesema bado kuna mazungumzo na timu pamoja na wachezaji wenyewe hivyo haitakuwa rahisi kuwataja kwa majina.
Kuhusu mwenendo wa Ligi Ndayiragije amesisitiza kwamba Ligi imekuwa ngumu kwa kila timu imejipanga kuhakikisha wanafanya Vizuri msimu Huu.
“Ligi ipo vizuri naona timu nyingi zimejipanga na ushindani upo vizuri, nimegundua msimu huu timu nyingi zimeamua kuwatumia vijana, ukishakuwa na Vijana wengi lazima changamoto iwepo na ndio maana unaona kasi ipo juu ni kitu kizuri kwa nchi na kwa mpira wa Tanzania,” amesema.
Mpaka sasa KMC imethibitisha kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Simba na Stand United Elias Maguri aliyekuwa anakipiga na AS Kigali ya nchini Rwanda kabla ya kuvunja mkataba.