- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
- Yanga na Rekodi iliyoshindikana
- Ratiba ya Mechi zote Ligi Kuu Tanzania
UMwekezaji mkuu wa klabu bingwa nchini Simba SC, Mohamed Dewji amesema kuwa tayari ametumia zaidi ya Tsh.12 bilioni ndani ya kipindi kisichopungua mwaka mmoja, pia ameweka wazi kuwa klabu hiyo ina madeni mengi makubwa hivyo anahitaji kupata hati za umiliki wa majengo ya klabu na mali nyingine.
Simba ilikuwa na mafanikio kiasi katika msimu uliopita baada ya kushinda tena kikombe cha ligi kuu na kufika hatua ya nane bora katika michuano ya Caf Champions League.
Kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya baadhi ya wanachama wa klabu hiyo na tajiri huyo kijana kuhusu kukabidhiwa hati na mali nyingine za klabu. Wanachama wanaona ni kama wataporwa klabu yao na kwa namna inavyoonekana wapo watu ndani ya klabu hawana imani na MO.
Kutumia zaidi ya bilioni 12 ndani ya mwaka mmoja na kushinda tu kikombe cha ligi huku wakifanya vibaya katika michuano ya Kagame Cup, FA, na kushindwa kufika walau fainali ya vikombe kama vya Mapinduzi Cup na SportPesa Super Cup ni ‘ufujaji’ mkubwa wa pesa.
MO wakati akipewa hisa za asilimia 49 kama mmiliki wa klabu hiyo aliwekeza Tsh 20 bilioni lakini ndani ya mwaka tu ametumia bilioni 12! Wakati akipigania kuichukua klabu hiyo nilisema ‘watu wa Simba watajuta’ je, majuto hayo ndio yanaanza sasa?
Kutumia bilioni 12 ndani ya miezi isiyozidi 16 ni ishara mbaya kwa Simba hii ya MO Dewji na ninaanza kuwa na mashaka makubwa na hatma ya klabu kwa ujumla kwa sababu kama uwekezaji wake ni bilioni 20 tu, inakuwaje atumie zaidi ya bilioni 12 ndani ya muda mfupi huku klabu ikiwa bado vilevile tu.
Bado hajajenga Hostel za timu, uwanja wa Bunju bado haujakamilika hivyo ukitazama juu juu tu unaweza kupata picha ya wapi klabu hiyo inapoelekea. Simba chini ya MO haijawahi kununua mchezaji yeyote kutoka klabu nyingine zaidi imekuwa ikiwasaini wachezaji huru tu, je hawa ndio wamekuwa ‘wakikomba’ pesa za MO?