SIJAWATAZAMA Nkana FC wakicheza, lakini hii ni timu yenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Zambia, na ni ´kongwe´ na kubwa kuliko mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara, Simba SC.
Nkana ´Mashetani Wekundu´ ndiyo mabingwa mara nyingi zaidi katika ligi kuu ya Zambia- wakitwaa mara 12. Wanamiliki uwanja wao mzuri-Nkana Stadium, huko mjini Kitwe. Timu hii inayotumia jezi za rangi nyekundu na nyeupe ilianzishwa mwaka 1935.
Nkana vs Simba mara ya mwisho…
Ni klabu tatu tofauti kutoka Zambia zimewahi kupangwa na timu za Tanzania katika michuano ya Caf ndani ya miaka hii 18 ya karne mpya, na michezo miwili kati ya Nkana vs Simba mwezi huu katika Caf Champions League Itakuwa ni ya nane kwa klabu za nchi hizo mbili majirani, na ni mara moja klabu ya Tanzania ilishinda katika michezo sita iliyopita.
´Wekundu wa Msimbazi´ ilikuwa klabu ya kwanza ya Tanzania Bara kukutana na klabu kutoka Zambia katika michuano ya Caf. Ilikuwa mchezo wa raundi ya kwanza ligi ya mabingwa Afrika mwanzoni mwa mwaka 2002.
Nkana wakianzia nyumbani ´waliipiga´ Simba 4-0, na licha ya kupoteza 3-0 Jamhuri Stadium, Morogoro katika mchezo wa marejeo, Red Devils walisonga mbele kwa ushindi wa jumla 3-4.
Machi 2004 ikiiwakilisha Tanzania katika michuano ya ligi ya mabingwa kwa mara nyingine Simba ilipangwa na timu kutoka Zambia katika raundi ileile waliyotolewa na Nkana miaka miwili nyuma. Safari hii Zesco United ambao wametwaa ubingwa wao wa saba wa ligi kuu Zambia mwaka huu.
Zesco klabu yenye uwanja mkubwa zaidi nchini Zambia ilikuja Dar es Salaam na kulazimisha suluhu-tasa kisha wakashinda 2-0 huko Lusaka na kusonga mbele.
Machi mwaka jana mabingwa mara 27 wa kihistoria Tanzania Bara, Yanga SC walikutana na Zanaco kutoka Zambia katika raundi ya kwanza Caf Champions League na mshindi wa jumla baada ya dakika 180 alikuwa akifuzu hatua ya makundi.
Yanga iliyokuwa na majeruhi wengi huku wachezaji wakiwa hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu ililazimishwa sare ya kufungana 1-1 na walienda Zambia na kuendeleza rekodi mbovu ya klabu za Tanzania si tu kutolewa na klabu za Zambia, bali kutofunga goli lolote katika ardhi ya Zambia.
Simba wameshindwa kufunga goli lolote katika ardhi ya Zambia katika michezo yao miwili iliyopita na Jumamosi hii watakuwa huko kujaribu kuvunja mwiko huo vs wababe wao Nkana Red Devils.
Nani mshindi?
Utabiri wangu
Nkana 4-0 Simba
Nitatoa sababu kesho Ijumaa. Paschal Wawa ni mahiri na ngome yake itaivusha Simba makundi? Chama ni bora?